Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amempongeza Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kwa ushindi wake katika nafasi hiyo na kuahidi ushirikiano wa dhati katika harakati za kuimarisha demokrasia nchini.
Kupitia chapisho lake katika mtandao wa X, Dorothy Semu ameandika: “Nakupongeza Ndugu Tundu Lissu kwa kushinda uchaguzi na kuwa Mwenyekiti wa chama chako cha CHADEMA. Kuchaguliwa kwako kunakufanya pia uwe Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Nikiwa Makamu wako huko, nakukaribisha sana katika uongozi wa TCD”
Dorothy Semu ameongeza kuwa ACT Wazalendo iko tayari kushirikiana na CHADEMA chini ya uongozi wa Lissu katika mapambano ya kuimarisha demokrasia.
“Nikiwa Kiongozi wa ACT Wazalendo nakuhakikishia ushirikiano wa dhati katika kupigania demokrasia ya nchi yetu,” amesema.
Aidha, Semu amempongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kwa kukamilisha muda wake wa uongozi na kuonesha mfano wa ukomavu wa kisiasa.
“Pia nakupongeza ndugu Freeman Mbowe kwa kukamilisha uongozi na kuachia demokrasia ichukue mkondo wake ndani ya chama chako. Nakutakia heri katika maisha yako ya ustaafu,” ameongeza.
Uchaguzi wa Tundu Lissu kama Mwenyekiti wa CHADEMA umeendelea kupokelewa kwa pongezi kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa, huku ukisifiwa kwa uwazi na haki uliodhihirisha.