Katika kukabiliana na changamoto za vitendo vya kikatili vinavyowakumba vijana, ikiwemo mila potofu kama ukeketaji na tohara isiyo salama, Shirika la Grumet Fund limeanza kutoa elimu kwa vijana wa kike na wa kiume ili kuwalinda dhidi ya madhara hayo.
Sambamba na juhudi hizo, shirika hilo pia linatoa elimu kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii, kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana unaotokana na matumizi mabaya ya teknolojia hiyo.
Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Serengeti, wilayani Serengeti mkoani Mara, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Grumet Fund, Frida Mollel, amesema kuwa shirika hilo limechukua hatua hiyo baada ya kushuhudia wasichana wakikumbwa na changamoto za ukeketaji, ndoa za utotoni, na kunyimwa haki ya kupata elimu.
Mollel ameeleza kuwa dhamira yao ni kunusuru kundi hili la vijana ambao wanakabiliwa na hatari kubwa, hasa katika maeneo ya vijijini. Kwa mwaka 2024 pekee, zaidi ya vijana 5,000 wamepatiwa elimu hiyo, huku shirika likiendelea kufikisha elimu kwa shule na vijiji vinavyozunguka mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumet.