Na Theophilida Felician, Kagera.
Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za maji na nishati (EWURA CCC) mkoa wa Kagera limebainisha kuwa katika juhudi zake za kutoa elimu kwa wananchi limefanikiwa kuwafikia jumla ya wananchi 9168 kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024.
Hayo yamesemwa na Afisa Msaidizi huduma kwa wateja na utawala, Anadorice Komba akizungumza na Jambo TV tarehe 23 Julai 2024 katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Manispaa ya Bukoba.
Afisa huyo ameeleza kwamba njia zilizowezesha kuwafikia wananchi hao ni pamoja na kutoa elimu kwenye mikutano ya wananchi inayoandaliwa na viongozi wa serikali za mitaa, kutembelea shule, vyuo vya kati, kutoa elimu kwenye shughuli za wadau wanapokuwa wamewashirikisha, kutoa elimu kupitia klabu kadhaa zilizoanzishwa na baraza hilo na wengine kufika moja kwa moja ofisini  ikiwa ni sambamba na kupiga simu.
Kupitia juhudi hizo, wananchi wamekuwa wakijitokeza kueleza changamoto zao kutokana utumiaji wa huduma za maji na nishati ambapo EWURA CCC imekuwa ikipokea changamoto hizo na kuzifikisha kwa watoa huduma na hatimaye kutatuliwa.
Kwa kipindi cha 2023 na 2024 kati ya malalamiko 287 yaliyoripotiwa 152 yanahusu umeme, 125 maji na malalamiko 10 ya mafuta.
“Katika malalamiko haya ya umeme tunashukuru kwamba mengi yameweza kutatuliwa na watoa huduma na mengi yalihusiana na madaraja ya watumiaji, wengine mita zinakuwa na shida, wengine wamelipia hawaunganishiwi umeme kwa wakati, yako mengi haya ni baadhi. Na kwenye umeme hapa malalamiko yaliyokwenda kwa mdhibiti ni manne na haya ni mabadiliko makubwa kwa sababu mwaka uliopita wa 2022/ 2023 tulikuwa na malalamiko zaidi ya 30 yaliyokwenda kwa mdhibiti ambao ni EWURA kwa hiyo kutoka malalamiko hayo hadi kushuka kwa kiwango hiki ni hatua kubwa mno kwa mtoa huduma ya umeme” Amesema Anadorice Komba.
Aidha amefafanua kuwa wanapowafikia wananchi zaidi ni kuwakumbusha namna ya kutambua haki na wajibu wao katika matumizi ya huduma hizo.
Amewasisitiza wananchi kutokukaa kimya pale wanapoona kuna tatizo kwenye huduma, watoe taarifa kwa watoa huduma au katika taasisi hiyo ambayo itashughulikia taarifa hiyo kwa ukaribu ili kutatuliwa.
Hata hivyo amehitimisha akiwakumbusha watoa huduma kufanyia kazi kwa wakati taarifa za wananchi wanapokuwa wamewajuza kuhusu lolote linalowakabili kwani hiyo itasaidia kupunguza kiwango cha malalamiko kwao huku akisisitiza kwamba wao kama EWURA CCC wataendelea kutimiza wajibu ipasavyo katika kuwafikia wananchi kama ilivyo dhamira ya serikali juu ya kuzitatua kero za wananchi.