Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zilizoanza kutumika Jumatano Juni 05, 2024.
Katika mchanganuo wa bei hizo mpya, bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kwa upande wa Dar es Salaam imeshuka kwa Shilingi 52.72 na kufikia Shilingi 3,261 kwa lita moja, ikilinganishwa na bei ya mwezi uliopita huku dizeli ikishuka hadi Shilingi 3,112 kutoka Shilingi 3,196.
Kulingana na taarifa ya EWURA, mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Juni 2024 yamechangiwa na kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa petroli na asilimia 7.77 kwa dizeli, na kuongezeka kwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa 1.4%.
Sababu zingine ni kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa wastani wa asilimia 2.06 kwa petroli na asilimia 8.51 kwa dizeli katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 7.07 kwa petroli na asilimia 25.24 kwa dizeli katika Bandari ya Tanga.