Latest Posts

FAIDA ZA MIRADI YA UBIA YA NHC NA WAWEKEZAJI BINAFSI

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuchukua hatua za kimkakati katika kuhakikisha maendeleo endelevu kwa kuimarisha utekelezaji wa miradi ya ubia baina yake na sekta binafsi. Mfumo huu wa ubia, uliotokana na Sera ya Ubia iliyozinduliwa mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho mbalimbali hadi mwaka 2022, umebuniwa ili kuhakikisha rasilimali za Shirika, hasa ardhi, zinatumika kwa tija na kuleta manufaa kwa pande zote. Hatua hizi zinalenga pia kukuza uchumi wa taifa kwa kuvutia uwekezaji wa kimkakati kutoka kwa sekta binafsi na umma.

Kwa miaka mingi, NHC imekuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa makazi na majengo ya kibiashara. Hata hivyo, kuongezeka kwa mahitaji ya makazi bora na miundombinu ya kisasa kumehitaji Shirika kuongeza mbinu bunifu za utekelezaji wa miradi. Wataalamu kutoka NHC, wanaeleza kuwa mfumo wa ubia umeonesha kuwa njia bora ya kufanikisha malengo haya, hasa kwa kutekeleza miradi mikubwa bila kutegemea rasilimali za kifedha za Shirika pekee.

“Miradi ya ubia ni miradi ambayo NHC timeizindua kwa lengo la kuwekeza viwanja vyetu ambavyo unakuta majengo yake yamechakaa sana, kwahiyo kutokana na namna ambavyo miradi mingine tunayotaka kuitekeleza ina gharama kubwa, kwahiyo tunachagua baadhi ya viwanja tunaingia ubia na wawekezaji binafsi”, ameeleza Mtaalamu kutoka NHC.

Moja ya maeneo muhimu ya mfumo huu ni utaratibu wa kutangaza viwanja vinavyotarajiwa kuendelezwa kwa njia ya ubia. Viwanja hivi hutangazwa kupitia njia rasmi, vikielezwa kwa undani kuhusu ukubwa wake, matumizi yaliyokusudiwa, na vigezo vya kuviendeleza. Wawekezaji hupewa fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao ya miradi ambayo yanapaswa kueleza kwa kina aina ya ujenzi unaokusudiwa, michoro ya awali, makadirio ya gharama, na mapato yanayotarajiwa.

Aidha, Shirika linaacha mlango wazi kwa wawekezaji wenye maono maalum kuomba kuendeleza viwanja ambavyo havijatangazwa rasmi. Hii imeongeza ubunifu na kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa miradi. Wawekezaji wanahimizwa kuzingatia mpango mkakati wa Shirika na mahitaji ya jamii husika kabla ya kuwasilisha maombi yao.

Katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango bora, NHC hufanya uchunguzi wa kina wa sifa za wawekezaji. Uchunguzi huu unahusisha ukaguzi wa hali ya kifedha ya mwombaji, uzoefu wake wa kiufundi, uhalali wa kisheria, na uwezo wake wa kutekeleza mradi kikamilifu. Hatua hii inalenga kupunguza hatari za kiuwekezaji na kulinda maslahi ya Shirika na wadau wake.

“”Mbia anatakiwa aambatanishe uthibitisho wa kuonesha kuwa ana fedha, kwasababu sisi tumeweka kigezo kwamba unapoomba kiwanja fulani labda chenye thamani ya Shilingi bilioni mbili, thamani ya mradi isipungue mara nne ya bilioni 2 (bilioni 8), kwahiyo sasa maana yake aende akabuni jengo linaloanzia Shilingi bilioni nane, kwahiyo akishabuni atuletee sisi tutaangalia kama ana huo uwezo bayana”, ameeleza.

Mfumo wa ubia unaofuatwa na NHC umejumuisha aina mbalimbali za ushirikiano, kulingana na mahitaji ya kila mradi. Aina moja maarufu ni ile ambapo Shirika linachangia ardhi pekee kama mtaji na mbia anachangia gharama zote za uendelezaji. Hii imetengeneza fursa ya Shirika kushiriki kwenye miradi mikubwa huku likihifadhi rasilimali zake nyingine kwa miradi ya baadaye.

Ubia mwingine ni ule unaojumuisha kuchangia ardhi na fedha. Katika mfumo huu, NHC na mbia wanashirikiana katika ujenzi kupitia kampuni maalum itakayoshughulikia mradi husika. Mfumo huu ni muhimu katika miradi mikubwa yenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni 50, na ambapo faida za uwekezaji zinapaswa kufikia viwango vya juu vya mapato na urejeshaji wa gharama ndani ya muda mfupi.

Mfumo wa kujenga, kuuza, na kugawana mapato pia umepata umaarufu mkubwa. Katika aina hii ya ubia, Shirika na mbia wanashirikiana katika ujenzi wa mradi, kisha mali zinazojengwa kuuzwa na mapato kugawanywa kwa uwiano uliokubaliwa awali. Mfumo huu unahakikisha kuwa Shirika linapata mapato makubwa, mara mbili ya thamani ya ardhi yake, huku mbia akinufaika kutokana na uwekezaji wake wa awali.

“Tunapompa mtu ajenge tunafaidika kwa kuwa tuna Sera ya Ubia inayoeleza namna gani tutagawana mapato lile jengo likishakamilika, tunaanza na mgawanyo wa asilimia 25 ya NHC kwa 75 ya mwekezaji jengo litakapokamilika kwa muda wa miaka 10, baada ya miaka 10 inakuwa mgawanyo wa hisa 50 kwa 50 halafu baada ya miaka 15 inakuwa mgawanya wa asilimia 75 ya Shirika la nyumba, mbia anakuwa na 25. Kwahiyo tunaamini baada ya miaka 15 anakuwa amerejesha fedha zake alizowekeza, kwahiyo atabaki na asilimia 25 kwahiyo sisi shirika tutakuwa tumebaki na asilimia 75; hiyo ni jumla baada ya miaka 25. Halafu nyingine baada ya miaka 10 ya kwanza ile 50 kwa 50, anakaa miaka mingine mitano sisi Shirika tutakuwa ja 60 yeye atabaki na 40 na tutaendelea hivyo mpaka mwisho”, ameeleza.

Kwa wawekezaji wanaotaka fursa za muda mrefu, mfumo wa upangaji wa muda mrefu umebuniwa. Huu unahusisha upangaji wa ardhi kwa kipindi kisichozidi miaka 30, ambapo mbia huendeleza kiwanja na kuendesha mradi kwa muda wa mkataba. Mwisho wa kipindi hicho, mali yote hurejeshwa kwa NHC. Aina hii ya ubia imelenga zaidi uwekezaji wa kibiashara na kuhakikisha matumizi bora ya ardhi za Shirika.

Katika kuboresha zaidi utekelezaji wa miradi, NHC imeweka vigezo madhubuti vya kuidhinisha miradi. Hii inahusisha viashiria vya utendaji, kama vile viwango vya mapato (IRR) visivyopungua asilimia 12, thamani ya mradi kuwa angalau mara nne ya thamani ya ardhi, na muda wa kurejesha gharama kutopindukia miaka 12. Hatua hizi zimeongeza uwajibikaji na ufanisi wa miradi yote inayotekelezwa chini ya mfumo wa ubia.

Mbali na hayo, Shirika limehakikisha kuwa ardhi zake hazitumiwi kama dhamana ya mikopo, hatua inayolinda rasilimali zake dhidi ya hatari za kifedha. Aidha, mikataba yote ya ubia huingiwa tu na makampuni au taasisi zilizosajiliwa rasmi, jambo linaloongeza uaminifu katika utekelezaji wa miradi.

Shirika limeweka wazi dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi na umma. NHC inahimiza wawekezaji kuwasilisha mapendekezo yao wakiwa na lengo la kuendeleza viwanja au majengo yanayoendana na mpango wa maendeleo wa taifa.

Huu ni mfano mzuri wa jinsi mashirika ya umma yanaweza kushirikiana na sekta binafsi katika kuleta maendeleo ya kiuchumi. Kwa kufungua milango ya uwekezaji, Shirika linasaidia kukuza uchumi wa nchi, kuongeza fursa za ajira, na kuimarisha miundombinu.

NHC inabaki kuwa mshirika wa kuaminika kwa wawekezaji wenye maono ya maendeleo ya muda mrefu. Kwa mfumo huu wa ubia, Shirika linatoa mfano wa jinsi rasilimali za umma zinavyoweza kutumika kwa tija kubwa, huku zikinufaisha pande zote na kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!