Katika jitihada za kuhakikisha Tanzania inafanikisha malengo manne ya kizazi chenye usawa, Jukwaa la Wanawake Wanaelimu wa Afrika, Zanzibar (FAWE Zanzibar) linasaidia wanawake Zanzibar kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi.
Kwa ushirikiano na UN Women Tanzania, FAWE Zanzibar inaunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Kuharakisha Maendeleo ya Kiuchumi kwa Wanawake Vijijini (JPRWEE). Mpango huu unalenga kuhakikisha ustawi wa wanawake vijijini na kulinda haki zao.
Utekelezaji wa mpango huu unajumuisha utoaji wa mafunzo kwa wanawake ili kuwasaidia kupata ujuzi wa biashara, elimu ya kifedha, na fursa za mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara zao. Katika Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo mradi huu unatekelezwa, wanawake wameweza kuongeza ajira, kuboresha kipato cha kaya, na kupunguza utegemezi kwa waume zao.
Wanufaika wa mradi wameeleza kwamba umeweza kuwasaidia kuanzisha biashara ndogo ndogo kama vile kuuza bidhaa za kilimo, ushonaji, na uzalishaji wa bidhaa za nyumbani kama sabuni na mishumaa. Hata hivyo, mradi huu haujafaidisha wanawake pekee; wanaume pia wamepata manufaa kupitia mradi huu, ambao umewezesha kufikiwa kwa haki na usawa wa kiuchumi.
Assaa Hassan Khamis, mwanakikundi cha upishi, SUBIRA INA MALIPO kutoka shehia ya uzi, Mkoa wa Kusini Unguja, alieleza mafanikio aliyopata kutokana na mafunzo ya upishi, ambayo yamewezesha kujiajiri mwenyewe na kumsaidia mke wake majukumu ya kupika.
Mwanakombo Nyange Shamata kutoka kikundi cha UROA SACCOS amesema wamepata mikopo inayowasaidia kununua vifaa vya ukulima wa Mwani, rasilimali kuu ya uchumi wao.
Shida Hassan Mambo kutoka kikundi cha TUPENDANE, kilichopo Uroa wilaya ya Kati Zanzibar, alisema kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha, wanawake wengi wameweza kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi, kuweka akiba, na kupanga matumizi yao vizuri. Hii imechangia kukua kwa biashara zao.
Hata hivyo, bado kuna changamoto katika soko la Mwani. Arabia Fauzi Pandu kutoka kikundi cha Mwani cha USALAMA WETU alisema kwamba bei inayowekwa na serikali kwa kilo ya mwani ni Shilingi 1,000, lakini wanunuzi hununua kwa Shilingi 700, hali inayowasababishia maumivu ya kiuchumi.
Afisa tathmini na ufuatiliaji FAWE Zanzibar, Shaban Suleiman, alisema mradi unawawezesha wanawake wa vijijini kiuchumi kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali, biashara, na mikopo kutoka serikalini kwa maendeleo yao zaidi.
Silvia Lanzarini, Afisa Ufuatiliaji na Mtaalam wa Programu kutoka UN Women, alihimiza wajasiriamali wanawake kuweka akiba ya fedha katika vikundi vyao ili waweze kupata mikopo zaidi inayosaidia kutatua changamoto za vikundi vyao na jamii inayowazunguka.
Programu ya Kizazi Chenye Usawa (2021-2026) inajumuisha afua nne: kuanzisha na kuendeleza vituo vya malezi na makuzi ya watoto; kuongeza uwekezaji katika usambazaji wa maji, umeme, na nishati mbadala yenye kutunza mazingira; kuongeza kazi zenye staha kwa kuendeleza biashara na urasimishaji wa biashara za wanawake; na kuboresha upatikanaji na matumizi ya teknolojia nafuu na zinazofaa ili kuongeza uwezo wa wanawake wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani wa soko la ndani na nje.