Uongozi wa taasisi ya kusaidia watu wenye ulemavu “Foundation for Disabilities Hope (FDH) wamekabidhi tuzo ya Cheti cha pongezi kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kutambua jitihada za kuunga mkono kundi la watu wenye ulemavu na makundi maalumu katika jamii ikiwamo walemavu nchini.
Hayo yamefanyika katika makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Arusha na kumkabidhi na cheti cha pongezi Kamishna wa Uhifadhi, Shirika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Juma Kuji kwa kutambua mchango wa shirika katika kusaidia watu wenye ulemavu na makundi maalumu katika jamii ikiwamo walemavu.
Aidha, kikao hicho kililenga kudumisha uhusiano uliopo kati ya TANAPA na FDH pamoja na kujadili maswala mbalimbali juu ya watu wenye ulemavu ikiwemo kampeni ya Niache Niishi, Utalii Jumuishi’ ambayo itahamasisha watalii kwenda kutalii hifadhi za Taifa.
Mozzah amesema dhima ya Foundation for disabilities Hope ni kuhamasisha watu wenye ulemavu kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea vivutio vya utalii ambapo italisaidia Taifa kupata mapato ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
FDH wamelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kazi kubwa ya kusimamia maliasili za Taifa pamoja na kusaidia watu wenye ulemavu katika jamii.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mozzah Mauly pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Maiko Salali na wafanyakazi wa FDH ndio waliotembelea ofisi hizo za TANAPA ambapo Salali ameeleza kujivunia sana  kwa TANAPA kuyashika mkono makundi ya watu yenye ulemavu.