Tangu kuitishwa na baadaye Jeshi la Polisi kupiga marufuku maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyokuwa yametarajiwa Septemba 23.2024 kumeshuhudiwa mijadala na mabishano ya hoja kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, ambapo kila mtu amekuwa akieleza kile anachokiona kuhusu sakata hilo lililohitimishwa kwa kushuhudiwa viongozi na wanachama wa chama hicho karibu 50 wakishikiliwa na Jeshi la Polisi
Katika mtazamo na mapokeo ya maandamano hayo ambayo pamoja mambo mengine, kwa takribani juma moja sasa marufuku ya Jeshi la Polisi imeenda sambamba na kufanyika kwa doria na oparesheni kali kwenye kila kona ya jiji la Dar es Salaam kama sio Tanzania kwa ujumla wake
Licha ya uwepo wa marufuku ya Jeshi la Polisi, lakini mjadala mpana unaanzia pale ambapo wengi walitarajia kuona pengine wafuasi wengi wa chama hicho wakijitokeza kukabiliana na Jeshi la Polisi, sambamba na kuhakikisha wanaandamana kama ilivyokuwa wito wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe.
Kitendo cha wafuasi na wanachama wa chama hicho kuingia mitini kimeonekana kuwakwaza wengi na wengine kuibua maswali lukuki kuhusiana na namna CHADEMA na wafuasi wake inavyokosa nguvu ya kuishikiniza dola, kwa kuwa wamemtelekeza Mwenyekiti na baadhi ya watu, huku wengi wao ikiwa bado haijafahamika sababu iliyowalazimu ‘kuingia mitini’
“Maandamano yanahitaji watu, watu hawajajitokeza, swali; ni uwoga au CHADEMA haivutii?, kama ni uwoga, na people’s power hakuna bargaining power ya CHADEMA ni nini?, bila ya bargaining power CHADEMA wataweza kuishinikiza CCM (Chama cha Mapinduzi) walete mabadiliko ya mfumo?” -Fatma Karume
Mwanaharakati Fatma Karume ni miongoni mwa wadau waliojitokeza hadharani kuwashukia na kuwakosoa vikali baadhi ya viongozi, wafuasi na wanachama wa CHADEMA kwa kutojitokeza kwao kushiriki maandamano, huku akitumia nafasi kubwa kumpongeza Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe na viongozi wengine waliojitokeza ingawa waliishia mikononi mwa Jeshi la Polisi
Andiko hilo liliamsha hisia na mawazo mseto kutoka kwa wafuasi wa CHADEMA na hata vyama vingine, bila kusahau wale ambao si wanasiasa wote wameshuhudiwa wakiingia kwenye mjadala huo
Mwanaharakati wa mitandaoni na kada wa CHADEMA Martine Maranja Masese ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumjibu Fatma Karume kwa kuandika yafuatayo;
“Kama kweli CHADEMA ingelikuwa haivutii tusingeona nguvu iliyotumika kuwazuia, silaha za kivita dhidi yao, kwani kwako watu wanaanza wangapi?, wamekamatwa zaidi ya watu 50 kutokana na hayo maandamano, viongozi wakuu wa CHADEMA wamekamatwa, wapo mahabusu leo (wakati huo), kwa nini wamekamatwa?, mapenzi?, serikali imetumia hadi akina Mwamposa kulaani maandamano” -Martin
Mjadala umekuwa mpana sana kila mmoja akimjibu Fatma Karume kwa vile anavyoona inafaa lakini yeye mwenyewe ameendelea na msisitizo wa kuwa CHADEMA imemtelekeza na kumuacha Mbowe akiandamana mwenyewe
“Naona wana CHADEMA wengi wanasema CHADEMA inavutia, sawa nakubaliana na ninyi 37-45 za kura ni nyingi na ni mvutio mkubwa, swali linalofuata mbona hamlijibu?, bila ya people’s power bargaining chip ya CHADEMA kuleta mabadiliko ni nini?, je CHADEMA inaweza kuwatoa uwoga Watanzania?” -Fatma Karume
Pitapita yangu kwenye mitandao ya kijamii nikiangaza namna mapokeo ya ujumbe wa Fatma ambaye pia ni mwanasheria nimekutana na chapisho la Wakili Tito Magoti akimjibu Fatma Karume kwa kueleza yafuatayo;
“Je, ni kazi ya CHADEMA kuwatoa uoga Watanzani?, CHADEMA sio jando eti litawapa ujasiri au JKT kwamba itawapa ukakamavu, CHADEMA isn’t in a bargain wth anyone maana hata mazingira ya kufanya hivyo hayapo, hatuna siasa bali dola inayoamua kila kitu” -Tito
Hata hivyo wapo wale wanaoamini kuwa CHADEMA imefanikiwa kwenye maandamano hayo bila kujali nini kimetokea.