Latest Posts

G55: KUSHIRIKI UCHAGUZI KUTAHUISHA UHAI WA CHADEMA NA KUIMARISHA MAPAMBANO YA MABADILIKO

Kundi la G55 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limeeleza kuwa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 ni hatua muhimu kwa ajili ya kuimarisha mshikamano wa wanachama, kuhuisha uhai wa chama na kuendeleza harakati za kisiasa, huku likisisitiza kuwa mabadiliko ni mchakato unaohitaji msimamo wa kimkakati na si kujitoa kwenye mapambano.

John Mrema, mmoja wa wajumbe wa kundi hilo, amesema kuwa licha ya changamoto nyingi zilizopo katika mfumo wa uchaguzi, zikiwemo kasoro za kikatiba, kisheria, na hujuma kutoka kwa chama tawala CCM, bado kuna nafasi ya kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana nazo kupitia ushiriki wa uchaguzi.

 

“Kushiriki uchaguzi kutasaidia kuimarisha na kuendeleza umoja na mshikamano wa Chama, wanachama na wananchi, kutahuisha uhai na kuendeleza nguvu, hamasa na harakati za Chama,” amesema Mrema.

Ameeleza kuwa vitendo vya kihuni kama vile kuzuia mawakala, kunyima fomu wagombea, au kuingiza kura feki si miongoni mwa mambo yaliyohalalishwa kisheria, bali ni matendo yanayokwenda kinyume na sheria na hivyo yanaweza kupingwa kupitia mbinu sahihi za kimkakati.

“Vitendo hivyo si halali kisheria, bali ni uhuni unaofanywa na CCM na serikali yake. Kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa ya kuja na mikakati madhubuti ya kukabiliana na vitendo hivyo moja kwa moja,” amesema.

Mrema ameikumbusha CHADEMA kuwa chaguzi za kihistoria kama ile ya mwaka 2015 zilifanyika chini ya mazingira haya haya ya kisheria na kikatiba, lakini chama kilipata mafanikio makubwa kwa kuwa kilijipanga na kuwa na wagombea sahihi.

“Tujiulize, nini kilichosababisha CHADEMA mwaka 2015, pamoja na tume na sheria zilezile, kikapata kura za urais asilimia 40 na kufikisha wabunge 73? Utaona kwamba tulikuwa na wagombea sahihi,” alisema Mrema.

Amesisitiza kuwa badala ya kukimbia uchaguzi, chama kinapaswa kuutumia vyema kama fursa ya kujijenga, kuweka wagombea sahihi na kujenga mshikamano wa ndani, huku kikiendelea kusukuma mbele hoja ya mabadiliko ya kweli ya mfumo wa uchaguzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!