Kundi la G55 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limeonya kuwa mpango wa kutoshiriki uchaguzi mkuu iwapo hakutapatikana mabadiliko ya kisiasa (reforms) unaweza kuligharimu chama hicho kwa kiasi kikubwa, likionya kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri uhai, mvuto, na mustakabali wa chama hicho.
John Mrema, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Aprili 6, 2025 kwa niaba ya kundi hilo, amesema kuwa matokeo ya kushindwa kuzuia uchaguzi yatakuwa ni kutoshiriki uchaguzi, jambo ambalo lina athari nyingi kwa CHADEMA.
“Katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari, Makamu Mwenyekiti wa Chama, Mhe. John Heche, amethibitisha kuwa ikiwa hakutakuwa na reforms, basi Chama hakitoshiriki uchaguzi,” amesema Mrema.
Ameeleza kuwa iwapo CHADEMA haitoshiriki uchaguzi, itakumbwa na madhara kadhaa, ikiwemo kupoteza viongozi na wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na urais, ubunge, na udiwani, kudhoofika kwa mvuto wa chama kwa umma, hali itakayowaacha wananchi wakikikwepa kutokana na ukosefu wa uelekeo wa kisiasa, kukosa ruzuku ya serikali, ambayo ni muhimu kwa kuendesha shughuli za chama, jambo litakaloathiri uhai wake na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Athari zingine alizozitaja ni kushuka kwa hamasa ya wanachama kuchangia chama, kwa kuwa hawatoweza kushiriki katika kinyang’anyiro cha kisiasa, na kukosa fursa ya kujijenga kupitia kampeni, hali itakayowakatisha tamaa watiania wa nafasi mbalimbali ambao hutegemea uchaguzi kujitangaza na kujijenga.
“Kutoshiriki uchaguzi kutakipotezea Chama uhusika wake kwa umma (relevance) na kuanza mporomoko wa kisiasa unaoweza kukifikisha hatua ya kudhohofika kabisa,” ameongeza Mrema.
Aidha, amesema tayari kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya chama kuhusu suala hilo, na endapo chama hakitashiriki uchaguzi, mpasuko huo utakuwa wazi zaidi na wa madhara makubwa.