Katika uchaguzi mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) uliofanyika Aprili 5, 2025 visiwani Zanzibar, Geofrey Kiliba, mwanafunzi kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ametangazwa rasmi kuwa Rais mpya wa TAHLISO kwa mwaka wa uongozi wa 2025/2026.
Kiliba ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura nyingi kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAHLISO, ambao wanawakilisha serikali za wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini Tanzania.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Kiliba amewashukuru wajumbe kwa kuonesha imani kubwa kwake na kuahidi kuwa kiongozi mwenye ushirikiano, uwazi, na maadili ya hali ya juu.
“Nitakuwa kiongozi mwenye masikio makubwa na mdomo mdogo. Nipo tayari kusikiliza hoja na haja zenu. Sote tuna ndoto za kuwa viongozi, lakini leo naomba mtangulize maono ili nitatimize ya kwetu sote,” amesema Kiliba kwa unyenyekevu.
Wajumbe wengi waliohudhuria mkutano huo wameeleza matumaini yao makubwa juu ya uongozi mpya, wakisema kuwa Kiliba anaonesha dira, maono na ari ya kweli ya kuleta mabadiliko chanya ndani ya TAHLISO.
Ushindi huu unakuja wakati TAHLISO inakabiliwa na majukumu makubwa ya kuwa sauti imara ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini, ikihitaji uongozi thabiti katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi.