Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, ametoa wito mzito kwa mamlaka nchini akitaka Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antiphas Lissu, aachiwe huru mara moja ili arejee kuendelea na majukumu yake ya kisiasa.
Akizungumza na televisheni ya mtandao ya Saut Digital kuelekea Februari 9, 2026- siku ambayo kesi ya Lissu inarejea mahakamani baada ya takribani miezi mitatu, Heche amesisitiza kuwa msimamo wa chama hicho haujabadilika na hautabadilika.
Heche amebainisha kuwa ujumbe wa CHADEMA kwa sasa ni mmoja na uko wazi; kumuachia huru mwanasheria huyo msomi kwani kesi inayomkabili haina mashiko kisheria.
“Ujumbe wetu ni ule ule kwamba hiyo kesi inayokabiliwa nayo mwenyekiti ni kesi ya uongo, ni kesi ya kubuni, haitakiwi kuwepo. Kwa hiyo ujumbe wetu ni ule ule kwamba tunataka mwenyekiti aachiwe, awe huru arudi kufanya shughuli zake. Hatuna ujumbe zaidi ya huo. Chama chetu kifunguliwe kwa sababu kipo kisheria, mwenyekiti wetu aachiwe arudi kufanya shughuli zake, kwa hiyo huo ndio ujumbe wetu”, amesisitiza Heche.
Makamu Mwenyekiti huyo amekiri kuwa kuendelea kuwekwa ndani kwa Tundu Lissu kunaleta changamoto na mkanganyiko katika uongozi wa chama, huku akiongeza kuwa hali hiyo inaambatana na mashambulizi mengine ikiwemo kuzuiliwa kwa shughuli za chama na kukamatwa kwa wanachama mikoani na wilayani.
Licha ya shinikizo hilo, Heche amesema CHADEMA iko imara kuliko wakati wowote kwani imeshavuka kiwango cha kuwa taasisi ya kwenye makaratasi na sasa imekuwa ni imani ndani ya mioyo ya watu. Alitaja mtandao wa misingi 46,000 nchi nzima kama kielelezo kuwa chama hicho kimeshajikita mizizi ambayo haiwezi kung’olewa na utawala wowote.
Ameitaja historia ya vyama kama ANC nchini Afrika Kusini vilivyopitia mazingira magumu na kufutwa kisheria lakini vikaendelea kuishi ndani ya watu, akisema hiyo ndiyo hatua ambayo CHADEMA imefika kwa sasa.
Heche amewataka wananchi na wanachama wa CHADEMA wasikate tamaa wala kuogopa pindi wanapoona viongozi wao wanapata misukosuko ya kisheria. Amehitimisha kwa kusema kuwa “hakuna njia rahisi kuelekea uhuru” na kwamba CHADEMA itaendelea kupambana hadi haki itakapopatikana.