Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetoa taarifa kwa umma kufuatia uvumi unaosambaa kuhusu kusitisha safari za treni ya umeme aina ya EMU – Electric Multiple Unit (Mchongoko) kutokana na changamoto za umeme.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha TRC, Fredy Mwanjala ameeleza katika taarifa iliyotolewa Novemba 6, 2024 kuwa tangu kuanzishwa kwa safari za treni zinazotumia nishati ya umeme mnamo Juni 14, 2024, hakujawahi kutokea changamoto yoyote ya umeme ambayo ingeathiri uendeshaji wa treni hiyo.
TRC imefafanua kuwa tukio la hivi karibuni la kusitisha safari lililotokea Novemba 3, 2024, halikusababishwa na changamoto za umeme bali ni kutokana na hujuma iliyosababisha kukatika kwa nyaya (catenary) zinazohusiana na mfumo wa usambazaji wa umeme.
TRC imeongeza kuwa tayari baadhi ya wahusika wa tukio hili wamekamatwa na hatua stahiki zimechukuliwa ili kufikisha suala hilo kwa vyombo husika vya sheria.
Shirika limehakikishia wananchi kwamba treni ya Mchongoko iko salama na haina hitilafu yoyote ya kiufundi. Aidha, TRC imewahakikishia wananchi kuwa litatoa taarifa rasmi kwa umma pale ambapo changamoto yoyote itakapotokea, na hivyo kuwataka wananchi kutoamini taarifa zisizo sahihi zinazozagaa mitandaoni.
Mwisho, TRC imewashukuru abiria kwa uvumilivu wao na kuwahimiza kuwa na subira katika kipindi hiki cha mwaka mmoja cha majaribio, huku ikisisitiza umuhimu wa kushirikiana na Tanesco ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme unaendelea kuwa wa uhakika kwa treni za umeme.