Kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ametoa andiko linaloibua mjadala wa mkwamo mkubwa wa kisheria na kikatiba nchini, akidai kuwa kwa sasa Mzanzibari hana mahali pa kwenda kudai haki yake ya kikatiba linapokuja suala la uchaguzi wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano.
Kauli hiyo ya Zitto aliyoiwasilisha Jumatano Januari 28, 2026 kupitia mtandao wa X inakuja siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Zanzibar (Masjala Kuu ya Tunguu), kutoa uamuzi uliotupa nje maombi 19 ya wagombea wa ACT-Wazalendo waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 2025.
Zitto amechambua mkanganyiko wa kisheria uliopo, akibainisha kuwa wakati Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar akiamua kuwa hana mamlaka ya kusikiliza kesi hizo na kwamba wenye mamlaka ni Mahakama Kuu ya Tanzania, bado kuna ukuta mwingine wa kisheria mbele ya Wazanzibari.
“Kanuni za mashauri ya Uchaguzi zilizosainiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania zinaelekeza kesi zote za uchaguzi kwa majimbo ya Zanzibar kufunguliwa kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar. Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ametoa hukumu kwamba Mahakama Kuu Zanzibar haina ‘jurisdiction’ kuamua kuhusu kesi za uchaguzi wa wabunge wa majimbo ya Zanzibar, kwamba wenye mamlaka ni Mahakama Kuu ya Tanzania. Mahakama Kuu ya Tanzania haina Masjala Zanzibar…majimbo yote 50 ya Zanzibar hayaangukii katika Masjala yoyote ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Kwa Hiyo, Mzanzibari mwenye kutaka kufungua shauri la uchaguzi wa wabunge hana pa kwenda”, ameandika Zitto Kabwe na kuongeza,
“Mzanzibari…hawezi kufungua shauri Mahakama Kuu ya Zanzibar kwasababu haina mamlaka, hawezi kufungua shauri Mahakama Kuu Masjala za Tanga au Mtwara au Dar es Salaam au Kigoma kwasababu majimbo ya uchaguzi ya Zanzibar hayapo kwenye Masjala hizo. Hawezi kufungua shauri Micheweni wala Wete, Makunduchi wala Tumbatu kwa sababu Mahakama Kuu ya Tanzania haina Masjala popote pale katika ardhi ya Zanzibar. milango yote ya haki imefungwa! Huu ndio Muungano tunataka Mzanzibari ajivunie nao? Hii ndiyo Katiba tunayosema inatoa haki kwa watu wote?”
Mkwamo huu umetokana na hukumu ya Jaji Haji Khamis iliyotolewa Januari 27, 2026, katika shauri la Moh’d Khamis Bussara na wenzake 18. Jaji Khamis amekubaliana na pingamizi la Serikali kuwa masuala ya uchaguzi wa Bunge ni “Mambo ya Muungano” na kwa mujibu wa Ibara ya 83 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977), Mahakama Kuu ya Tanzania ndiyo yenye mamlaka ya kipekee.
Licha ya utetezi wa Wakili Omar Said Shaaban kuwa kuwalazimisha Wazanzibari kufungua kesi Bara ni kuwanyima haki kwa gharama na umbali, Jaji alisisitiza kuwa kufuata mamlaka ya kikatiba si suala la urahisi wa mtu, bali ni amri ya sheria.