Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imepanga kupokea fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo siku ya Jumamosi, Septemba 13, 2025, saa nne asubuhi, katika ofisi za tume jijini Dar es Salaam. Wagombea waliopendekezwa na chama hicho ni Luhaga Mpina na Fatma Fereji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Juma Rahisi kwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu na ambayo Jambo TV imeithibitisha, wagombea wanatakiwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 20(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuwasilisha fomu zilizojazwa kikamilifu, picha nne za rangi zenye mandhari meupe, uthibitisho wa malipo ya dhamana ya Shilingi milioni moja, na fomu namba 10 ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.
Tume imeelekeza kuwa kila mgombea ataruhusiwa kuambatana na watu wasiozidi kumi (10) pekee, bila shamrashamra au maandamano ndani au nje ya jengo la tume.
Hatua hii inajiri siku moja baada ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, kutoa uamuzi kwamba Mpina ana haki ya kuendelea na mchakato wa kurejesha fomu ya kugombea Urais wa Tanzania.
Katika shauri Na. 21692/2025, Mahakama ilibainisha kuwa zuio lililowekwa na INEC Agosti 27, 2025, kwa kumzuia Mpina kurejesha fomu, lilikuwa kinyume cha sheria na Katiba.
Uamuzi huo, uliotolewa Septemba 11, 2025 na Jaji Abdi Kagomba, ulieleza kuwa waleta maombi- Bodi ya Wadhamini wa ACT Wazalendo na Luhaga Mpina walikuwa na haki ya kupewa nafasi ya kurejesha fomu kwa wakati. Hata hivyo, ombi lao la kulipwa fidia ya Shilingi milioni 100 lilikataliwa.