Na; Fred Owden
Iran imesema kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa wazi kwa usafirishaji wa kimataifa, lakini itawazuia kile ilichokiita “maadui” wake kutumia njia hiyo muhimu ya baharini, huku mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati ukiendelea kuongezeka.
Kauli hiyo ilitolewa Alhamisi na Ali Akbar Velayati, mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran Mojtaba Khamenei, kupitia ujumbe aliouandika katika mtandao wa kijamii wa X.
“Mlango-Bahari wa Hormuz uko wazi kwa dunia, lakini utabaki kufungwa kwa maadui wa watu wa Iran na kambi zao katika eneo hilo,” alisema Velayati, akisisitiza kuwa Iran itaendelea kudhibiti njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani.
Aliongeza kuwa matokeo ya vita vinavyoendelea kati ya Iran kwa upande mmoja na Israel pamoja na Marekani kwa upande mwingine, vitaamuliwa na mkakati wa Iran.
“Vita vitaisha kwa mkakati na mamlaka ya Iran, si kwa dhana zisizo halisi za washambuliaji,” alisema.
Kauli hizo zinakuja saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa uwezo wa kijeshi wa Iran umepungua kwa kiasi kikubwa, akidai kuwa taifa hilo limebakiwa na makombora “machache sana” na uwezo mdogo wa kutumia ndege zisizo na rubani.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa vita, Trump alisema anatarajia mapigano hayo kuendelea kwa muda wa wiki mbili hadi tatu zijazo, lakini akaashiria kuwa mgogoro huo unakaribia kumalizika.
Mlango-Bahari wa Hormuz ni njia nyeti ya kimkakati inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Hindi, na hupitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayosafirishwa kwenda mataifa ya Asia. Kauli ya Iran imezua wasiwasi kuhusu usalama wa usambazaji wa nishati duniani.
Mvutano katika eneo hilo umeongezeka tangu tarehe 28 Februari, baada ya Israel na Marekani kuanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,340, akiwemo aliyekuwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei. Hali ya usalama katika eneo hilo inaendelea kuwa tete, huku mataifa mbalimbali yakifuatilia kwa karibu uwezekano wa kuathiriwa kwa biashara ya kimataifa na usambazaji wa nishati.
CHANZO: TRT AFRIKA