Latest Posts

JONG UN AISHUTUMU MAREKANI KWA “UGAIDI WA KIDUNIA”; AAPIZA KUIFANYA NORTH KOREA NGUVU YA NYUKLIA ISIYOTINGISHIKA

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amezindua shambulio kali la maneno dhidi ya Marekani, akiishutumu Washington kwa kuendesha “ugaidi wa serikali na uchokozi” kote duniani, huku akitangaza rasmi kuwa nchi yake imefikia hatua ya “kurudi nyuma mwiko” kama nguvu ya nyuklia duniani.

Akihutubia Bunge la nchi hiyo (Supreme People’s Assembly) jana Machi 23, 2026, Kim alitumia mivutano inayoendelea Mashariki ya Kati kama kielelezo cha kile alichokiita “ubabe wa kijambazi” wa Marekani. Amesema Korea Kaskazini itachukua nafasi ya nguvu zaidi katika “umoja wa mataifa yanayopinga Marekani” ili kukomesha kile alichokiita njama za kibeberu.

Kim ameweka wazi kuwa usalama wa taifa lake hautategemea tena ahadi za kidiplomasia, bali utategemea silaha za nyuklia ambazo sasa zimeingizwa kwenye Katiba mpya ya nchi hiyo.

“Ugaidi wa kimataifa unaofanywa na Marekani unalazimisha taifa letu kuimarisha ulinzi. Utukufu na ushindi wa mwisho wa jamhuri yetu unaweza tu kuhakikishwa na nguvu kubwa zaidi ya nyuklia ambayo haitabadilika kamwe,” alisema Kim kwa msisitizo.

Katika mabadiliko makubwa ya kisiasa, Kim ameiita Korea Kusini kuwa ni “adui mkubwa na mwenye chuki zaidi,” akiondoa kabisa uwezekano wa muungano wa amani uliokuwa ukizungumzwa kwa miongo kadhaa. Ameishutumu Seoul kwa kuwa kibaraka wa Marekani na kikwazo kikubwa cha usalama katika rasi ya Korea.

Licha ya shutuma hizo za “ugaidi,” Kim ameacha mlango mdogo wa mazungumzo na utawala wa Donald Trump, lakini kwa sharti moja lisiloweza kujadiliwa: Marekani lazima iache matakwa ya kutaka Korea Kaskazini iachane na nyuklia (Denuclearization) kama sharti la kuanza mazungumzo na mazungumzo yoyote lazima yafanyike kwa kuheshimu hadhi ya Korea Kaskazini kama nchi inayomiliki silaha za nyuklia.

Shutuma hizi zinakuja wakati Korea Kaskazini ikiwa imeimarisha ushirikiano wake na Urusi, ikituma maelfu ya wanajeshi kusaidia vita vya Ukraine. Wachambuzi wanasema Kim anajiona kuwa na nguvu zaidi sasa kuliko wakati wa mikutano yake ya kwanza na Trump mwaka 2018 na 2019.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!