Latest Posts

IRAN YASISITIZA HAITAFANYA MAZUNGUMZO MOJA KWA MOJA NA MAREKANI CHINI YA SHINIKIZO

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema kuwa vitisho vya Marekani dhidi ya taifa lake “havitaleta matokeo yoyote”, baada ya Rais Donald Trump kuonya uwezekano wa hatua za kijeshi dhidi ya Iran.

“Wamarekani wanapaswa kuelewa kwamba vitisho havitafanikiwa wanapokabiliana na Iran,” Khamenei alisema Ijumaa katika hotuba yake ya kila mwaka ya Nowruz, sherehe ya Mwaka Mpya wa Kiajemi, iliyotangazwa mubashara kwenye televisheni.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa, “Wao (Marekani) na wengine wanapaswa kufahamu kuwa wakifanya lolote baya dhidi ya taifa la Iran, watajibiwa kwa nguvu kubwa.”

Mnamo Machi 7, Trump alisema kuwa alimwandikia barua Khamenei, akimtaka kuanzisha mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, huku akionya kuwa kuna uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi iwapo Iran itakataa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema Alhamisi kuwa barua hiyo ilikuwa zaidi ya tishio, ingawa pia ilionesha uwezekano wa mazungumzo. “Tunachunguza kwa kina maudhui ya barua hiyo, na tutajibu rasmi katika siku chache zijazo”.

Kulingana na ripoti ya tovuti ya habari ya Marekani, Axios, ikimnukuu afisa wa serikali ya Trump na vyanzo vingine, barua hiyo inaweka muda wa miezi miwili wa kufikia makubaliano mapya ya nyuklia. Hata hivyo, haijabainishwa ni lini muda huo utaanza au kuisha.

Kwa muda mrefu, Khamenei amepuuza wito wa Trump wa mazungumzo ya moja kwa moja, akisema kuwa rais huyo wa Marekani anajaribu kudanganya ulimwengu kwa kuonesha kuwa Marekani iko tayari kwa mazungumzo huku Iran ikionekana kutotaka kushiriki.

Trump, ambaye alianza muhula wake wa pili Januari 2025, amerudisha sera yake ya “shinikizo la juu” dhidi ya Iran. Wakati wa kipindi chake cha kwanza, Trump aliiondoa Marekani kwenye makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu ulimwenguni, na akairejeshea Tehran vikwazo vikubwa vya kiuchumi.

Kwa mwaka mmoja baada ya Marekani kujiondoa, Iran iliendelea kutekeleza makubaliano hayo, lakini baada ya muda ilianza kupunguza ahadi zake kwa kuongeza viwango vya urutubishaji wa madini ya uranium hadi asilimia 60.

Kiwango hiki kiko juu zaidi ya kiwango cha asilimia 3.67 kilichowekwa kwenye makubaliano ya awali, na kinakaribia asilimia 90 inayohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.

Juhudi za kufufua makubaliano ya nyuklia (JCPOA) zimegonga mwamba, huku Iran ikiendelea kushutumu Trump kwa sera zake zenye mkanganyiko. Araghchi amesisitiza kuwa Iran haitakubali mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani ikiwa bado iko chini ya shinikizo la vikwazo na vitisho vya kijeshi.

“Iran haitafanya mazungumzo moja kwa moja ikiwa inakabiliwa na shinikizo, vitisho, na vikwazo vilivyoimarishwa,” alisema Araghchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!