Latest Posts

ISSA GAVU: SERIKALI YA AWAMU YA NANE YALETA MAENDELEO MAKUBWA JIMBONI CHWAKA

Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Oganaizesheni, Issa Gavu, amesema Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imefanikisha maendeleo makubwa kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM.

Akizungumza Desemba 14, 2024, wakati wa kukabidhi msaada wa pikipiki 20 zenye thamani ya Shilingi milioni 72 na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Shilingi milioni 17, Gavu ameeleza kuwa juhudi za serikali zimeleta mageuzi makubwa katika miundombinu ya barabara, elimu, afya, na maji ndani ya Jimbo la Chwaka.

“Tumeshuhudia changamoto mbalimbali zikitatuliwa moja baada ya nyingine. Serikali imeonesha uthubutu wa kuwahudumia wananchi kwa mipango madhubuti na yenye matokeo chanya. Hili linaonyesha dhamira ya kweli ya CCM ya kuwatumikia Watanzania,” amesema Gavu.

Katika hafla hiyo, amekabidhi pia vifaa vya ujenzi, vitenge, fulana, kofia, vyarahani 100, na mashine za kuprintia, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 90. Mchango huu unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii, hususan vijana na wajasiriamali.

Akizungumzia uchaguzi ujao, Gavu ameeleza matumaini yake kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kushinda kutokana na rekodi yake ya mafanikio.

“Licha ya kuwepo vyama 19 vya siasa, hakuna chama kingine chenye uthubutu wa kuliongoza taifa letu kwa mafanikio makubwa kama CCM,” amesema.

Amewataka wananchi wa Chwaka kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana na kusisitiza umuhimu wa kujitokeza kwa wingi wakati wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.

“Hoja yetu tunaijibu kwa vitendo. Tunapaswa kujiandaa vizuri kuhakikisha daftari la wapiga kura linafanyiwa uboreshaji wa asilimia 100. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao,” ameongeza Gavu.

Pia amesisitiza kuwa miradi ya maendeleo ikiwemo vyuo vya ufundi, vituo vya elimu, na miradi ya wajasiriamali ni ushahidi wa dhamira ya CCM ya kuinua maisha ya wananchi.

“Yapo mambo tuliyokuwa tunakumbana nayo kama changamoto, lakini serikali hii imeonyesha dhamira ya kuyatatua. Mabadiliko tunayoyaona leo ni matokeo ya uongozi wa CCM,” amehitimisha.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!