Latest Posts

JAJI MKUU: JAMII IELIMISHWE KUHUSU USULUHISHI NJE YA MAHAKAMA

Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa ni vyema Wizara ya Katiba na Sheria kupitia kampeni ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria ya ‘Mama Samia Legal Aid’ ikaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za kufanya usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama ili kuepuka kutumia muda mrefu kusikiliza mashauri, kuepuka gharama kwa wanaohusika katika migogoro (Wadaawa) na kuepuka msongamano wa mashauri Mahakamani

Prof. Ibrahim amesema hayo katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa  Wizara ya Katiba na Sheria Jumanne Sagini wakati alipomtembelea Jaji Mkuu katika ofisi za Mahakama ya Rufani zilizopo Kivukoni, jijini Dar es Salaam Juni 20, 2024 kwa lengo la kufahamu majukumu na muundo wa muhimili wa Mahakama, kuimarisha mashirikiano baina ya Wizara ya Katiba na Sheria na muhimili wa Mahakama, sambamba na kujifunza namna walivyoweza kufanikiwa kwenye masuala ya miradi ya maendeleo na matumizi ya TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano).

“Katiba ya Tanzania katika kipengele cha utoaji haki, inasisitiza katika kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro, suala la kusuluhishwa kwa dakika thelathini linaweza kuchukua miaka zaidi ya kumi, zipo baadhi ya nchi ambazo zaidi ya asilimia tisini na tano (95%) ya mashauri yanaisha kwa njia ya usuluhishi, ni vyema sheria ielekeze kuwa, kabla ya suala kwenda Mahakamani lianze kwenye usuluhishi kwani kunajenga ukaribu na sio uadui”Ameeleza Prof. Ibrahim

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini ameupongeza muhimili wa Mahakama kwa kazi kubwa wanazofanya katika kusimamia utoaji haki kwa wananchi, kusimamia ujenzi wa Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini na pia kufanya mageuzi katika utendaji wa Mahakama ikienda sambamba na matumizi ya TEHAMA.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri Sagini amesema katika kipindi cha nyuma cha utendaji kazi wake kama Katibu Tawala, kumekuwa na changamoto  ya kamati ya maadili ya Mahakimu katika ngazi za wilaya na mikoa kutokutana na kufanya vikao, na limekuwa likisahaulika ambapo Jaji Mkuu Prof. Ibrahim amesema kuwa kwa sasa kamati hiyo ikiwa na Katibu wa Tume ya utumishi wa Mahakama imekuwa ikizunguka katika mikoa mbalimbali nchini  kwa lengo la kuzijulisha kamati za wilaya na mikoa namna ambavyo zinatakiwa kufanya kazi na kuzijengea uwezo zaidi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Msajili Mkuu wa Mahakama Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani George Hillary Herbet, Naibu Msajili Mahakama Kuu Venance Mlingi ambaye pia ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania na Hakimu mkazi Jovine Constatine ambaye pia ni Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!