Sakata la binti aliyedaiwa kubakwa na kulawitiwa na watu watano linaendelea kuchukua sura mpya na kuibua maswali lukuki baada ya Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Theopista Mallya kusema kuwa vijana wanaotuhumiwa kutenda tukio hilo la ‘kinyama’ walikuwa kama walevi/ wavuta bangi na kwamba muathirika wa tukio hilo (binti) alikuwa kama anajiuza/ kahaba
SACP Mallya ametoa kauli hiyo iliyoibua sintofahamu na mjadala usiokuwa na majawabu miongoni mwa jamii alipohojiwa na kampuni ya magazeti ya Mwananchi Communication Ltd ambapo katika maelezo yake amesema jalada la kesi hiyo limekamilika na kwamba leo, Jumatatu Agosti 19.2024 atafuatilia kuona kama litafikishwa Mahakamani.
Kuhusu madai ya kwamba vijana watano (5) wanaotuhumiwa kutenda kosa hilo wametumwa na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la ‘Afande’, Kamanda wa Polisi mkoa (RPC) Dodoma amesema uchunguzi wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa vijana hao hawakutumwa na askari yeyote na kwamba katika mahojiano vijana wenyewe wamekana kuagizwa na askari yeyote kama inavyoelezwa
“Neno askari (Afande) ni general (yaani la jumla) kwa kuwa hata Mgambo (Askari wa Jeshi la akiba) ni askari hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo” -SACP Mallya
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema jalada la kesi hiyo halijafikishwa ofisini kwake kwa kuwa bado linaendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi
Amesema anaamini suala hilo bado linaendelea kufanyiwa upelelezi na Jeshi la Polisi na kwamba ofisi yake Ina jukumu la kukamilisha upelelezi tu pindi litakapofikishwa kutoka kwa Jeshi la Polisi kabla ya kupelekwa Mahakamani
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa leo, Jumatatu Agosti 19.2024 na kampuni ya magazeti ya Mwananchi Communication Ltd imeeleza kuwa katika kufuatilia sakata hilo waandishi wake wamemtafuta pia Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai Tanzania (DCI) Kamishna wa Polisi (CP) Ramadhan Kingai ambaye alitoa maelekezo kuwa ili kupata majibu ya suala hilo watafutwe Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma SACP Theopista Mallya au Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime kwa ajili ya ufafanuzi
Katika taarifa hiyo, wamedai kuwa licha ya kuzungumza na Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma lakini waliendeleza jitihada za kumpata Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP Misime ambaye alipopigiwa simu hakupokea na kwamba hata alipotumiwa ujumbe mfupi kupitia mtandao wa What’sup aliusoma pasipo kurudisha majibu
Itakumbukwa taarifa ya mwisho iliyotolewa na Jeshi la Polisi Agosti 09.2024 kupitia kwa Msemaji wa Jeshi hilo DCP David Misime ilibainisha kuwa uchunguzi wake wa awali umebaini kuwa tukio hilo limefanyika mwezi Mei mwaka huu (2024) katika eneo la Swaswa, jijini Dodoma
Ambapo kupitia taarifa hiyo DCP Misime aliwataja baadhi ya watu wanaoshikiliwa kwa kudaiwa kutenda kosa hilo kuwa ni Clinton Damas anayefahamika kwa jina maarufu la Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nickson Jackson ambapo katika maelezo yake alibainisha kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwenye mikoa ya Dodoma na Pwani huku watuhumiwa wengine wawili (2) wakiendelea kutafutwa
Hata hivyo, tangu kutolewa kwa taarifa hiyo kumękuwa na ukimya hali inayoibua maswali na sintofahamu miongoni mwa jamii.