Jeshi la Polisi Tanzania limetoa tamko kutokana na malalamiko yanayoenea mitandaoni na vyombo vya habari ikiwamo Jambo TV ambayo iliripoti kwa kina kuhusu tuhuma za Mkuu wa Kituo cha Polisi Makete Mjini wilayani Makete, Mkoa wa Njombe, kumvunja mkono Levis Mahenge kwa kumpiga. Tukio hilo limeripotiwa kufanyika Oktoba 9, 2024, majira ya saa 12:30 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa siku ya Jumamosi Oktoba 19, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, jeshi hilo limeeleza kuwa baada ya tukio hilo kugundulika, hatua za kisheria na kinidhamu zimeanza kuchukuliwa dhidi ya Mkuu huyo wa Kituo cha Polisi.
“Baada ya tukio hilo kugundulika na Uongozi wa Polisi Mkoa wa Njombe, jalada lilifunguliwa na ushahidi ukakusanywa na uchunguzi umekamilika. Hivi sasa hatua za kinidhamu zinaendelea kukamilishwa dhidi ya Mkuu huyo wa Kituo na baadaye hatua za kisheria zitafuata kwasababu tuhuma anazokabiliwa nazo ni za kijinai”, ameeleza Misime.
Kama uliikosa taarifa hiyo kwa kina, inapatikana katika chaneli ya Youtube ya Jambo TV kupitia kiungo kifuatacho, https://youtu.be/Q9Dp8aHNGzY