Kampuni inayojihusisha na kilimo cha kahawa ya JJAD Kagera Farmers imeishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia bei ya kahawa kupanda bei hadi kufikia Shilingi 1,200 mwaka jana mpaka kufikia Shilingi 5,300.
Hayo yamesemwa tarehe 22 Agosti 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Dkt. Albert Katagira mara baada ya uzinduzi wa kongamano na maonesho ya 21 ya kahawa bora Afrika.
“Zao la kahawa kwa mwananchi wa Kagera sasa limekuwa mkombozi mkubwa na ninashukuru sana AFCA kuamua kuleta kongamano na maonesho ya kahawa Tanzania mwakani. Kongamano hilo litatusaidia sana kuongeza mbinu mpya za kulima zao hili na tutapata masomo mengi”, amesema Dkt. Katagira.
Aidha Dkt. Katagira amesema kuna umuhimu wa serikali kuwakopesha wakulima wa kahawa kwani kuandaa mashamba ya zao hilo kuna gharama kubwa sana.

“Kuendesha mashamba makubwa ya kahawa siyo kazi rahisi kwa hiyo, tunaomba serikali ione umuhimu wa kuwa inawakopesha wakulima mikopo midogo midogo ya kulima kahawa ili wakulima wengi wahamasike kulima zao hili,” amesema Dkt. Katagira.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa (TCB), Primus Kimaryo amesema kongamano la 21 litafanyika mwakani na ni fursa ya kipekee kwa wakulima wa kahawa kwani uzalishaji wa kahawa hiyo umekuwa ukiongezeka.
Amesema bodi ya AFCA iliamua kuwa kongamano lao la mwakani litafanyika jijini Dar es Salaam na itakuwa fursa ya kipekee kwa wakulima wa kahawa Tanzania kuonesha kahawa wanayozalisha kwa ajili ya kutafuta masoko ya zao hilo.
“Hii ni fursa kubwa kwa wakulima kutafuta masoko ya kahawa na kuongeza ubora wa kahawa kwa sababu bei ya kahawa duniani inazidi kuwa nzuri kwa hiyo wanapaswa kuitumia hiyo fursa kuyafikia masoko ambayo ni makubwa,” amesema Kimaryo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya AFCA, Amir Hamza amesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa kongamano na Maonesho ya 21 ya Kahawa Bora za Afrika (Afrika Fine Coffee Conference & Exhibitions) kuanzia 26 – 28 Februari, 2025, jijini Dar es Salaam.
Amesema kongamano na maonesho haya ni jukwaa kubwa zaidi la biashara ya kahawa barani Afrika, huvutia zaidi ya wadau wa kahawa 2,000 kutoka ndani na nje ya Afrika kila mwaka ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wafanyabiashara wa kahawa, wakaangaji wa kahawa na pia wadau kutoka wa sekta ya umma na binafsi, na wawakilishi wa serikali.
“Tanzania ni nchi yenye fursa kubwa katika katika sekta ya kahawa na kongamano na maonesho haya yanadhihirisha ubora wa kipekee wa kahawa za Afrika na pia yanaimarisha dhamira ya nchi za Afrika kukuza ukuaji na ushirikiano katika sekta ya kahawa Afrika”, amesema na kuongeza,
“Kauli mbiu ya Kongamano la 21 ni “Kuhuisha Ongezeko la Thamani” ambapo kwenye Kongamano patakuwepo na orodha ya wazungumzaji maarufu kimataifa na kikanda. Aidha Maonesho ya kahawa yatakayofanyika yataonesha ubunifu na maendeleo yaliyotokea hivi karibuni katika sekta ya kahawa,” amesema.
Amesema pia kutakuwepo warsha ambazo zitakuwa na majadiliano yenya tija, kutoa fursa za kipekee za kuonja na kutathmini kahawa na safari maalumu zitakazoandaliwa ili kujifunza kuhusu kahawa. Amesema katika kongamano na maonesho haya kutakuwepo na mashindano ya watayarisha kahawa Afrika (Barista Championship) na mashindano ya kahawa bora katika ukanda wa Afrika ili kuonesha vipaji na bidhaa bora zaidi za kahawa kutoka kote barani.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Chama cha Kahawa Bora Afrika (AFCA) linatarajiwa kufanyika mwezi wa pili mwakani na linatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya washiriki 2,000 ambao ni wadau wa biashara ya kahawa Afrika na maeneo mengine duniani.
Kampuni ya JJAD Kagera Farmers Limited iliyoko wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imekuwa ikiendesha kilimo cha kahawa aina ya Robusta kwenye mashamba yenye ekari 100.