Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amemshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, kwa mchango wake mkubwa katika kuwalea na kuwajenga kisiasa viongozi wa chama.
Kupitia mtandao wa X, Heche amejibu ujumbe wa Mbowe aliyewapongeza viongozi wapya wa CHADEMA baada ya uchaguzi uliohitimishwa Januari 22, 2025.
“Asante sana Mwenyekiti, umetujenga na kutulea, umeonesha demokrasia kwa kuongoza timu kusimamia uchaguzi wa wazi, huru na haki,” amesema Heche.
Makamu Mwenyekiti huyo mpya pia alimtaja Mbowe kama kiongozi ambaye historia ya Tanzania itamkumbuka kwa mchango wake wa kujenga demokrasia na mageuzi makubwa, akisema:
“Historia ya Tanzania itakukumbuka kama mtu uliejenga demokrasia na kuleta mageuzi makubwa kwenye Nchi na chama chetu.”
Mbowe, aliyemaliza muda wake kama Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, ameandika ujumbe wa pongezi kwa viongozi wapya wa chama, akiwemo Mwenyekiti mpya, Tundu Lissu. Katika ujumbe huo, Mbowe alisema:
“Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama chetu CHADEMA uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la Uongozi wa Chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele Chama chetu.”