Latest Posts

JOHN HECHE: CHADEMA NI IMANI, IKO MIOYONI MWA WATU NA HAIWEZI KUFUTIKA.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema kuwa chama hicho kimevuka hatua ya kisheria na sasa kimekuwa ni “imani” iliyojikita mioyoni mwa Watanzania, jambo linalofanya iwe vigumu kwa mamlaka yoyote kukifuta.

Akizungumza na televisheni ya mtandao ya Saut Digital muda mfupi kabla ya kurejea kwa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, inayotarajiwa kusikilizwa Februari 9, 2026, Heche amesisitiza kuwa CHADEMA iko imara licha ya kile alichokiita “mashambulizi ya kila upande.”

Heche amefananisha harakati za CHADEMA na zile za chama cha ANC nchini Afrika Kusini au kuenea kwa dini kuu duniani, akibainisha kuwa mashambulizi na mateso mara nyingi ndivyo huimarisha misingi ya mapambano.

“CHADEMA iko imeenea kila mahali kwenye nchi hii. Sasa unaiuaje? Yaani unaendaje kwenye kitu ambacho kimeshaingia mpaka kwenye imani za watu? Kila kijiji tuna uongozi”, amesema Heche na kuongeza,

“Wanaweza kusema wameki-disband kwenye makaratasi kwa kutumia msajili wakasema tumeifuta CHADEMA lakini CHADEMA haifutiki. Ndio maana nimekupa mfano wa ANC, ANC ilifutwa kabisa kwa miaka kadhaa ilikuwa ukiitaja ANC umevunja sheria Afrika Kusini lakini haikufutika kwasababu ilikuwa imeshavuka level hiyo ya kuweza kufutwa. Na sisi ndio level hiyo tuliyofika”.

Akifafanua juu ya uimara wa chama hicho, Heche amebainisha kuwa CHADEMA ina uongozi thabiti katika kila kitongoji (msingi) nchini kote. Ameeleza kuwa katika misingi yote 46,000 na shehia nchi nzima, kuna viongozi wasiopungua watano katika kila eneo, hali inayofanya mtandao wa chama hicho kuwa imara kiasi cha “kuitisha serikali dhaifu.”

Kuhusu kurejea kwa kesi ya Tundu Lissu baada ya miezi mitatu, Heche ametoa ujumbe mmoja; kuitaka serikali kumuachia huru mwenyekiti huyo akidai kuwa kesi inayomkabili ni ya “kubuni na uongo.” Amesema kuwa chama kinataka Lissu awe huru na CHADEMA iruhusiwe kufanya shughuli zake za kisiasa kwa mujibu wa sheria.

Makamu Mwenyekiti huyo amewataka wanachama na wapenzi wa CHADEMA kutokata tamaa wala kuogopa, kwani historia inaonyesha kuwa hakuna njia rahisi kuelekea uhuru wa kweli (no easy way to freedom).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!