Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja waandishi wa habari wawili wa Jambo TV na mmoja wa Chanzo TV waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kikazi wakati wa ‘kamatakamata’ ya jeshi hilo iliyotokea Jumapili ya tarehe 11 Agosti 2024 kwenye ofisi za CHADEMA mkoani Mbeya.
Taarifa iliyotolewa na TEF kupitia kwa Mwenyekiti wake Deodatus Balile imeeleza kuwa waandishi hao ambao ni Ramadhan Khamis na Fadhili Kirundwa wa Jambo TV, na mpiga picha wa Chanzo TV Francis Simba wanapaswa waachiwe bila masharti kwa sababu kuwapo kwao katika eneo la tukio haikuwa sehemu ya siasa bali kutekeleza majukumu yao huku ikieleza kuwa wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Mbalizi.
“Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inatoa haki ya watu kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya nchi. Sambamba na Katiba, Kifungu cha 7(1)(a)(b) na (c) cha Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kama ilivyorekebishwa mwaka 2023, kinatoa haki kwa waandishi wa habari kufanya kazi ya uandishi wa habari. Ni jukumu la waandishi wa habari kuhabarisha umma juu ya kila jambo linaloendelea, hivyo mwandishi hapaswi kukamatwa au kuadhibiwa kwa kufanya kazi hii”, imeeleza TEF.
TEF imelaani matukio ya kukamata waandishi wa habari ikieleza kuwa yanaharibu heshima kubwa ya Tanzania katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari aliyoijenga Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 kwa kurejesha uhusiano mzuri na vyombo vya habari.
“Sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania, tusingependa kuona Tanzania ikirejea katika enzi za giza za kamatakamata. Tunasema waandishi waliokamatwa waachiwe haraka”, imeeleza taarifa hiyo.