Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe linamshikilia Daniel Kafyulilo (39) mkazi wa Chaugingi halmashauri ya mji wa Njombe kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza (6) wa shule ya msingi Selestini iliyopo mkoani Njombe.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga ameweka wazi kushikiliwa kwa mtuhumiwa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wa ubakaji kumetokana na taarifa za raia wema wa mkoa huo walizozitoa kwa jeshi hilo kwa kushirikiana na wazazi wa mtoto huyo.
“Kwahiyo uchunguzi wa jarada hili unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa huyu atafikishwa mahakamani” amesema Banga.
Ametoa wito kwa wakazi wa Njombe kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kusisitiza wazazi kuzungumza na watoto wao kutembea makundi wanapoenda na kurudi shuleni.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa kumetokea ikiwa zimepita siku sita pekee tangu ulipotendeka ukatili huo Mei 22,2025 majira ya saa moja asubuhi,wakati mtoto huyo akiwa njiani kuelekea shuleni.