Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, Mei 23, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, amewavisha vyeo askari Polisi 208 ngazi ya Koplo, Sajenti na Sajini Meja wa Polisi.
Akizungumza na askari hao, Kamanda Kuzaga amewataka kudumisha nidhamu katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku na kuleta mabadiliko chanya ndani ya Jeshi la Polisi.
Aidha, Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa, Jeshi hilo linatambua mchango wa kila Askari na kwamba Polisi itaendelea na utaratibu wake wa kuwapandisha vyeo na kutoa zawadi mbalimbali kwa askari kutoka na utendaji unaozingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu.
Mmoja wa Askari aliyevishwa cheo Sajini Meja wa Polisi Benson Lucka wa Polisi Wilaya ya Mbeya amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura kwa kuwapendekeza na kuwapandisha vyeo kutokana na utendaji kazi wao.
Askari hao wamevishwa vyeo mbalimbali baada ya kupendekezwa na kisha kuhudhuria na kuhitimu mafunzo ya uongozi mdogo katika vyuo na Shule ya Polisi Tanzania (TPS) zamani ikijulikana CCP iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro.