Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema kuwa hali ya ulinzi jijini humo imeimarika kwa kiwango kikubwa tangu kabla ya Pasaka hadi sasa, na kwamba ongezeko la askari mitaani si jambo la kuwatia hofu wananchi bali ni hatua ya kulinda usalama wa wote.
Akizungumza na kituo cha habari cha BBC Jumatatu, Aprili 28, 2025, Muliro amesema Jiji la Dar es Salaam limepiga hatua kubwa katika kudhibiti uhalifu ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo matukio mengi ya kihalifu yalikuwa yakiripotiwa.
“Kama unaishi Dar es Salaam, tangu kabla ya Pasaka, wakati wa Pasaka na baada ya Pasaka, hali ya ulinzi imeimarishwa sana. sijui sisi kwenda mitaani au kupita mitaani kuimarisha masuala ya kiusalama sidhani kama hilo ni suala baya, askari ni wengi, tumeimarisha ulinzi na mji wetu uko salama,” amesema Muliro na kuongeza kuwa askari wameongezwa kwenye maeneo yenye viashiria vya hatari ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Alipoulizwa kuhusu madai ya polisi kuzingira nyumba za viongozi wa CHADEMA, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara John Heche na Mwenyekiti wa Taifa Tundu Lissu, Muliro amekanusha madai hayo.
“Sisi tunaimarisha ulinzi kwa watu wote bila ubaguzi, sasa ukiwa na mtazamo hasa dhidi ya jeshi ni mtazamo binafsi, lakini sehemu kubwa ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaona namna hali ilivyobadilika na kuimarika ya kiusalama katika jiji letu. Watu wa Kitunda, Mwanagati na Msongola wanafurahia uwepo wa polisi. Kama hali ingekuwa mbaya, viongozi wa CHADEMA wasingefanya mikutano zaidi ya 20 ndani ya wiki mbili hadi tatu zilizopita,” amesema.
Muliro amesisitiza kuwa watu wanaotoka maeneo ya nje ya jiji wanaweza kushangazwa na hali ya ulinzi, lakini wenyeji wanatambua mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na uhalifu, akibainisha kuwa usalama umepewa kipaumbele kikubwa na Jeshi la Polisi.