Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetoa wito kwa wababa na wazee nchini kuhakikisha wanawaunga mkono wake zao, dada zao na mama zao katika kipindi cha ujauzito na uzazi, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
‎Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Dkt. Dkt Emanuel Nuwas amesema ushiriki wa wanaume katika masuala ya uzazi ni muhimu si tu katika kutoa moyo kwa wajawazito wakati wa kujifungua, bali pia katika malezi ya watoto hasa katika siku 1000 za mwanzo za maisha yao.
‎
‎Amesisitiza kuwa wababa na wazee wana jukumu kubwa katika kuhakikisha mama na mtoto wanapata lishe bora, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika afya na maendeleo ya mtoto anayezaliwa.
‎Kamati hiyo ilitembelea hospitali hiyo tarehe 27, siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo iliwakabidhi vifaa muhimu wazazi na watoto wachanga, pamoja na kujionea utoaji wa huduma za afya katika hospitali hiyo.
‎Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Zeyana Abdallah Hamid,ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya pamoja na kuanza kwa mchakato wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.
‎
‎Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Sarah Ludovick, amesema kwa sasa watoto wanazaliwa katika mazingira salama kutokana na upatikanaji wa vifaa tiba na dawa muhimu.

