Sekta ya afya nchini imepiga hatua kubwa ya upatikanaji wa vifaa pamoja na vifaa tiba kutokana na umahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa vya uchunguzi wa magonjwa na kupunguza safari za kufuata huduma hizo nje ya nchi.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema hayo Juni 09, 2025 wakati akipokea na kukabidhi nepi (Softcare) kwa watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General) zilizotolewa na kampuni ya Doweicare Limited inayosimamiwa na Zarinah Hassan (Zari) ambaye ni balozi wa bidhaa hizo.
“Mafanikio yote ya sekta ya afya yamesababishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha katika ngazi zote, sasa hivi kila kituo kipo vizuri, tuna wataalamu wa kutosha na tuna ile programu ya madaktari wa Mama Samia imewafikia Watanzania wengi ambao wanaendelea kufaidika na programu hiyo,”amesema Waziri Mhagama.
Amesema, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha inazidi kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na kwa wakati kwa kununua dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi ya msingi.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kila mwaka takribani akina mama milioni 2.4 hupata ujauzito na kati ya hao asilimia 85 hujifungulia hospitalini na kufanya ongezeko la watoto ambao wanahitaji uangalizi wa karibu kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za afya.
“Katika makuzi watoto huwa na uwezo wa kutambua hali ya kutaka kujisaidia wafikapo umri wa miaka miwili hadi mitatu kwa wakati wa mchana, umri wa miaka mitano kwa wakati wa usiku, hivyo wale wenye umri mdogo zaidi nepi hizi zitawasaidia,” amesema Waziri Mhagama na kuongeza,
“Sote tunajua kuwa watoto wetu ambao wanakuwa bado hawajajitambua tumekuwa tukiwavisha nepi si tu kwamba katika kusaidia usafi na faraja ya mtoto, bali pia ni nyenzo muhimu katika kuzuia maambukizi”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwakuwa gharama za kutibu magonjwa hayo ni kubwa na lazima yatibiwe na wataalam wenye ubingwa na bobezi ambapo serikali imeendelea kusomesha wataalam hao.