Latest Posts

KAMATI YA BUNGE YA MAJI NA MAZINGIRA YAIDHINISHA RANDAMA YA BAJETI YA WIZARA YA MAJI 2026/27

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imejadili na kuidhinisha Randama ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Majadiliano hayo yamefanyika Bungeni jijini Dodoma yakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga, ambapo wajumbe walipitia kwa kina mapendekezo ya bajeti pamoja na vipaumbele vilivyowasilishwa.

Wasilisho la randama hiyo limefanywa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti wa Wizara ya Maji, Tedy Mwaijumba, kwa niaba ya Waziri wa Maji.

Kwa mujibu wa randama hiyo, Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwemo kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji vijijini 867, ujenzi wa mabwawa 35, pamoja na miradi 220 ya maji mijini.

Aidha, wizara itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Mpango wa Mtandao wa Taifa wa Usambazaji Maji (Gridi ya Maji ya Taifa).

Vipaumbele vingine ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa (dira janja), kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, kuboresha uendelevu wa huduma za maji, kuongeza uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kupunguza upotevu wa maji, pamoja na kuibua vyanzo mbadala vya fedha kwa ajili ya miradi ya maji. Pia, wizara imepanga kuimarisha taasisi zake pamoja na mfumo wa uratibu wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Kuidhinishwa kwa randama hiyo kunatoa fursa kwa Wizara ya Maji kuandaa Hotuba ya Bajeti kwa mwaka 2026/2027 itakayowasilishwa katika Bunge la Bajeti.

Akizungumza baada ya kuidhinishwa kwa randama hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameishukuru Kamati ya Maji na Mazingira inayoongozwa na Jackson Kiswaga pamoja na wajumbe wake kwa mchango wao, na kuahidi kuwa wizara itazingatia maoni yote yaliyotolewa katika kuboresha hotuba ya bajeti ijayo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!