Latest Posts

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA UBORESHAJI WA HUDUMA KATIKA BANDARI ZA TANZANIA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa mafanikio makubwa katika kuboresha huduma za bandari nchini, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali.
 
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso, amesema hayo baada ya ziara ya kukagua utendaji kazi katika Bandari ya Dar es Salaam. Ameeleza kuwa wamejionea maboresho makubwa katika bandari mbalimbali kama Dar es Salaam, Mtwara, na Tanga, pamoja na ujenzi wa bandari kavu katika maeneo mbalimbali ili kupunguza msongamano wa mizigo.
 
“Tunaipongeza TPA kwa usimamizi mzuri wa bandari baada ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta hii. Serikali imetoa fedha nyingi kwa ujenzi wa bandari mpya, ikiwemo Bandari ya Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa, ambayo inagharimu mabilioni ya shilingi,” amesema Kakoso.
 
Kakoso amesisitiza kuwa maboresho ya bandari ni nyenzo muhimu kwa uchumi wa taifa, kwani zinachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ameeleza kuwa katika Bandari ya Dar es Salaam, idadi ya meli zimeongezeka kutokana na kupungua kwa muda wa kushusha mizigo, hali inayorahisisha shughuli za biashara na usafirishaji.
 
Akizungumzia maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam, Kakoso amesema kuwa miradi kama Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP) inahakikisha uboreshaji wa miundombinu, upanuzi wa lango la meli, na uimarishaji wa mifumo ya umeme.
 
Pia, amesisitiza kuwa uwekezaji wa kampuni kama DP World katika bandari hiyo unatoa fursa kwa TPA kuwekeza zaidi kwenye bandari nyingine kama Mtwara na Tanga, pamoja na bandari kavu za Kwala (Pwani) na Uhumwa (Dodoma).
 
Aidha, Kamati hiyo imeshauri TPA kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi kuharakisha ujenzi wa reli inayoingia moja kwa moja bandarini ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo. Pia, wamependekeza mamlaka hiyo kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa maeneo ya hifadhi kwa upanuzi wa bandari katika miaka ijayo.
 
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dkt. Baraka Mdima, amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi na wadau wengine katika kuimarisha huduma za bandari, huku akibainisha kuwa Bandari ya Dar es Salaam inahudumia nchi jirani kama Rwanda, Burundi, DR Congo, Zambia, Malawi, Uganda, na Zimbabwe.
 
Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa wizara hiyo Bw, David Kihenzile amempongeza Rais Samia kwa kuruhusu uwekezaji mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam uliosababisha maeneo mbalimbali ya uboreshaji huduma ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kisasa.
 
“Matokeo haya tunayoyaona yanatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuweka mazingiza bora ya kuvutia wawekezaji na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na uboreshaji wa bandari mbalimbali hapa nchini”, amesema Bw. Kihenzile.
 
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Gallus Abed, amesema maboresho hayo yameleta mabadiliko makubwa, ambapo muda wa kushusha mizigo bandarini umepungua kutoka wastani wa siku 7-10 hadi siku tatu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!