Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda ametoa tahadhari kwa wafanyabishara na walipa kodi wote kwa ujumla wake kutambua kuwa hakuna ofisa yeyote wa mamlaka hiyo mwenye nguvu ya kusamehe kodi kama ambavyo baadhi yao wanadhani, badala yake wanapaswa kufahamu kuwa suala la kodi ni suala la kisheria na linapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.
Mwenda amezungumza hayo mapema Alhamisi Julai 18, 2024 alipokuwa kwenye kikao kazi kilichowakutanisha TRA na viongozi wa wafanyabiashara Tanzania chini ya uratibu wa TPSF (Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania), kilichofanyika Johari Rotana Hotel, jijini Dar es Salaam.
Amesema anafahamu kuwa kuwa, kinachofanyika na baadhi ya maafisa wa TRA wasiokuwa waaminifu ni kuhairisha kutokusanya kodi kwa wakati huo ili kutengeneza mazingira ya rushwa, jambo ambalo amedai kuwa linasababisha madhara kwa mfanyabiashara husika siku za usoni kwa kuwa pindi atakapofanyiwa ukaguzi hapo baadaye itabainika kuwa hajalipa kodi kwa muda mrefu na hivyo kujikuta akikabIliwa na mzigo mkubwa zaidi
Amesema mkakati wa mamlaka hiyo ni kumaliza kabisa mnyonyoro wa upokeaji wa rushwa kwa maafisa wake, na kwamba wale wachache watakaobanika kujihusisha na matendo ya rushwa kwa namna moja au nyingine hatua kali zitachukuliwa dhidi yake
Aidha, Mwenda ametoa wito kwa wafanyabishara na walipa kodi kwa ujumla wake kutotengeneza mazingira ya rushwa kwa maafisa wa TRA kwa kuwa anafahamu kuwa baadhi ya walipa kodi wamekuwa wakiwashawishi maafisa wa TRA wapokee rushwa ili wapate nafuu za kikodi jambo ambalo amedai kuwa halikubaliki kwa kuwa linachafua taswira ya mamlaka hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula ameishauri serikali kupitia TRA kuwa na mipango ya muda mrefu ya ukusanyaji mapato na vyanzo vyake ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii hususani kwa wafanyabiashara ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakidai kuwa TRA inalazimika kutumia nguvu kwenye ukusanyaji wa kodi kupitia ‘task force’ na kuongeza kodi kwenye bidhaa mbalimbali kiholela ili kukidhi mahitaji ya kibajeti kwa mwaka husika wa fedha, jambo ambalo amedai kuwa linawaumiza wafanyabiashara.
Amependekeza kuwapo kwa mpango mkakati wa miaka mitano wa ukusanyaji kodi ili kujua kama nchi itapata wapi kodi badala ya kusubiri miezi michache kabla ya bajeti.
Akizungumza katika kikao hicho, Ngalula amesema kama nchi mara zote imekuwa ikifahamu mwaka unaofuata kuna bajeti inayopaswa kupitishwa hivyo ni vyema kuwapo kwa maandalizi badala ya kusubiri miezi michache kabla ya bajeti kufika.
“Tuwe na mkakati kuangalia kodi yetu itatoka wapi inaamana kodi ya mwaka 2028 tunaanza kuijadili leo lakini kama tutakuwa tunakaa tunasubiri imebaki miezi michache bajeti ya mwaka 2025/2026 tunasubiri Desemba ndiyo tunaanza kuitana kwenye kikosi kazi kujadili kodi inapatikana wapi mwisho wa siku tunaishia kurudisha mlemle” Amesema Ngalula.
Amesema kuwa ni jambo ambalo halikubaliki kusikia Tanzania ina walipa kodi milioni 2 pekee kwenye nchi yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 61. Katika kuongeza wigo wa walipakodi, ametaka kuwekwa urahisi na motisha ili watu waweze kurasimisha biashara zao na kuanza kulipa kodi.
“Mimi ni mama ntilie nafanya biashara chini ya mwembe sina tozo za OSHA, TBS, sina mtu wa afya atakayenisumbua lakini nimejikusanya nifungue kaofisi kadogo asubuhi TRA ameshafika mlangoni. Mtu akiwa ana bodaboda nyingi hahitaji leseni lakini nikisema nafungua kampuni ni kosa la jinai,” Amesema Ngalula.
Kikao hicho kinafanyika ili kusikiliza changamoto zilizopo katika ufanyaji wa biashara Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alipokuwa akimuapisha Julai 3, 2024 kuongoza nafasi hiyo.
Baada ya kumuapisha Rais Samia alimtaka Mwenda kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi ili kuweka mazingira sawa ya biashara.