Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wananchi na viongozi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Ilala kuendelea kuunga mkono kampeni ya usafi wa kila Jumamosi, akisisitiza kuwa ushiriki wa kila mmoja ni muhimu kwa afya na ustawi wa jamii.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi wa kila Jumamosi lililofanyika kwenye fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Dengu, Mpogolo amesema kampeni hiyo inalenga kulinda mazingira na kudhibiti magonjwa ya mlipuko hasa katika kipindi hiki cha mvua.
“Kwa pamoja tukitimiza wajibu wetu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, tutapunguza magonjwa ya mlipuko na kujenga jamii yenye afya,” alisema Mpogolo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutunza fukwe za bahari na rasilimali zake, akisema zinachangia kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Fukwe ni utajiri wa jamii, ni maeneo ya kiuchumi na kitega uchumi kwa vijana wetu. Tukiangalia usafi wa fukwe tunapambana pia na mabadiliko ya tabianchi,” aliongeza.
Zoezi hilo la usafi limeanzia Makutano ya Barabara ya Kamata, kupitia Utumishi, Terminal 1 na kuhitimishwa eneo la Dengu.
Walioshiriki ni pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Ilala Elihuruma Mabelya, Katibu Tawala wa Wilaya Charangwa Sulemani, viongozi wa mitaa, wakandarasi na wananchi.