Kampuni inayojihusisha na ujenzi, chakula, usafiri na nishati kutoka Tanzania ya Amsons Group inatarajia kupata hadi asilimia 100 ya hisa za kampuni ya Bamburi Cement ya Kenya zenye thamani ya dola milioni 180.
Kampuni hiyo imetoa ofa ya lazima ya kuichukua Bamburi ambayo itafanya muamala wake kuwa moja ya mikataba mikubwa ya uwekezaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikionesha nia ya kikundi hicho kuwekeza katika moja ya kampuni kuu za Kenya zinazotambulika kwa umma kitaifa, kimataifa na kuwa na thamani ya wazi ya soko, na zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi (NSE).
Kampuni ya Amsons Group, biashara inayomilikiwa na familia na inayofanya shughuli zake nchini Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi ilisema siku ya Jumatano kwamba imetia saini ya ofa ya kudumu na Bamburi Cement.
Mkurugenzi Mkuu wa Amsons Group Edha Nahdi alisema mpango uliopendekezwa utaongeza nafasi ya kundi hilo hilo katika sekta ya saruji Afrika Mashariki kama sehemu ya maendeleo ya kiuchumi ya kikanda na maadili ya ushirikiano wa soko.
“Tuna mipango mizuri ya kuimarisha uwekezaji wetu nchini Kenya kupitia Bamburi. Ofa yetu ya kupata hisa Bamburi ni sehemu ya mpango wetu wa upanuzi wa soko la kampuni na itaashiria kuingia rasmi kwa Amsons Group katika soko la Kenya ambapo tunapanga kufanya uwekezaji katika viwanda vingine katika miezi ijayo” Ameeleza Nahdi.
Kampuni ya Amsons Group kupitia kampuni yake tanzu ya Amsons Industries Limited ya Kenya, imependekeza ofa kwa umma ambayo itawafanya wanahisa wa Bamburi kulipwa Shilingi za Kenya 65 ambazo ni sawa au takribani dola 0.51 kwa kila hisa.
Bamburi inamilikiwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya Holcim ya Uswizi kupitia kampuni zake mbili za uwekezaji ambazo ni Fincem Holding Limited na Kencem Holding Limited zikiwa na hisa za pamoja ambazo ni asilimia 58.3.
“Makubaliano haya ya kuuza hisa zetu za Bamburi Cement yanaendeleza mkakati wa Holcim wa kupanua uongozi wetu katika masoko yetu ya msingi kama kiongozi wa kimataifa katika suluhisho la ujezi wenye ubunifu na endelevu” Ameeleza Martin Kriegner, mkuu wa Holcim Asia, Mashariki ya Kati na Afrika.
Amsons Group ilianzishwa mwaka 2006 nchini Tanzania na sasa ina zaidi ya dola bilioni 1 katika mauzo ya kila mwaka.
Shughuli zake kuu za biashara kihistoria zilihusisha uagizaji wa mafuta kwa wingi na bidhaa za petroli chini ya chapa ya rejareja ya Camel Oil Tanzania.
Kwa muda sasa, Amsons imeendelea kukuza wigo wake katika sekta ya viwanda ikitengeneza saruji tani 6,000 kwa siku ambazo zimetengenezwa pia kupitia kituo cha saruji cha Mbeya ilichokimiliki hivi karibuni.