Kampuni ya Sandaland Fashion Wear Limited, maarufu kwa jina la Sanda au Sandaland the Only One, imemtaka Ally Shaban Kamwe kulipa fidia ya Shilingi bilioni 3 za Kitanzania kwa madai ya kuchafua chapa (brand) na jina la kampuni hiyo kupitia maneno inayodai kuwa ya uzushi yaliyosambazwa kwenye video iliyorekodiwa na kusambazwa mwezi Novemba mwaka huu.
Kupitia barua rasmi ya madai iliyotolewa na wanasheria wa Sandaland, kampuni hiyo imedai kuwa maneno yaliyotolewa na Kamwe si ya kweli na yameathiri vibaya biashara yao. Barua hiyo, iliyotumwa rasmi kwa Kamwe tarehe 26 Novemba 2024, imeeleza kuwa video ya uzushi iliyoenezwa kupitia vyombo vya habari ndani na nje ya Tanzania, imechafua sifa ya kampuni hiyo na kuathiri mahusiano yake ya kibiashara na wateja.
Kampuni ya Sandaland inajulikana kwa kusambaza vifaa vya michezo kwa Simba Sports Club, Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), na mashirika mengine mengi mashuhuri. Katika video hiyo, Kamwe anadaiwa kusema kuwa bidhaa za Sandaland hazina ubora, na kwamba viongozi wa Simba Sports Club waligomea uzinduzi wa jezi mpya kwa sababu ya kutoridhika na bidhaa hizo.
Sehemu ya maneno hayo ya uzushi, kama ilivyonukuliwa kwenye barua ya wanasheria wa Sandaland, ni: “nasikia viongozi wamemshambulia bwana Sanda, wamemshambulia sana Bwana Sanda, bwana Sanda wewe sisi tumechoka sana kutukanwa kila siku mitaani, tunachekwa tunadhalilishwa, vitu havina quality, na ndiyo maana hata uzinduzi wamemsusia ameenda kuzindua dukani kwake, ndio‘ nakwambia wamemsusia, sasa ndio aibu tu wamemsusia, na hata vijana wao wameambiwa nyie fanyeni tu promotion mechi ya mwanza, jezi msizungumzie tena, ni aibu huwezi promote tena kitu hiko.”
Sandaland imesema kuwa madai hayo hayana msingi na yameathiri sifa nzuri ambayo imeijenga kwa muda mrefu katika sekta ya mavazi na vifaa vya michezo. Wanasheria wa kampuni hiyo wamesema kuwa maneno hayo siyo tu yameleta athari ya moja kwa moja katika biashara, bali pia yamepunguza fursa za kibiashara za baadaye kwa kampuni hiyo.
“Maneno haya yamekuwa na athari kubwa kwa biashara ya mteja wetu, hasa kwa kuwa ni msambazaji rasmi wa Simba Sports Club, Timu ya Taifa, na wateja wengine mashuhuri,” imeeleza barua hiyo.
Sandaland imemtaka Kamwe kutimiza masharti matatu ndani ya siku saba tangu tarehe ya barua hiyo, ikiwa ni pamoja na kulipa fidia ya shilingi bilioni 3, kuomba radhi hadharani kwa uzushi uliofanyika, na kuhakikisha ombi hilo la radhi linatangazwa katika vyombo vya habari vyote vilivyoweka taarifa hizo za uzushi.
Aidha, barua hiyo imeonya kuwa endapo Kamwe hatatimiza masharti hayo ndani ya muda uliotolewa, kampuni hiyo imepanga kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yake, hatua ambazo zitahusisha gharama kubwa kwake.
Hatua hii inakuja wakati ambapo sekta ya michezo inazidi kuangaziwa kwa changamoto za biashara na ubora wa bidhaa zinazotolewa kwa wachezaji na mashabiki. Sandaland imesisitiza kuwa bidhaa zake ni za ubora wa hali ya juu, na kwamba madai ya Kamwe ni sehemu ya kampeni ya kuchafua jina lake bila ushahidi wa msingi.
Kampuni hiyo sasa inasubiri uamuzi wa Kamwe, huku ikionya kuwa haitasita kuchukua hatua za kisheria ili kulinda jina lake na maslahi ya biashara yake.