Latest Posts

KAWAIDA: VIJANA MKAOMBE MIKOPO YA 10% UVCCM TUMESHAELEKEZA

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Mohammed Ali Kawaida amewasihi vijana wasomi wanaohitimu elimu ya vyuo na vyuo vikuu kuchangamkia fursa ya mikopo ya Halmashauri ambayo imeboreshwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kawaida ameyasema hayo alipokua anahutubia wasomi wa seneti ya vyuo na vyuo vikuu UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam kwenye Mahafali ya Seneti hiyo tarehe 16 Juni 2024 Karimjee Hall Jijini Dar es Salaam.

“Sasa ile mikopo Dkt. Samia Suluhu Hassan ameirejesha ikiwa imeboreshwa, tukumbuke kuwa ile mikopo haina riba ni kwa ajili ya vijana wote na si ya kundi fulani fulani tu,  nendeni mkaombe ile mikopo na sisi UVCCM Taifa tushatoa maelekezo kwa viongozi wetu huko mikoani na wilayani mkifika huko mtapewa ufafanuzi na maelezo ya kutosha” Amesema Kawaida.

Aidha Kawaida amewasihi vijana wasomi wa Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu UVCCM mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.

“Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Vijiji na Vitongoji lakini pia tuna Uchaguzi Mkuu 2025 na sisi Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tumekubaliana kuwaunga mkono kwenye Uchaguzi huu nendeni mkachukue fomu mtuachie kazi ya kuwasemea kwenye Vikao”

Katika hatua nyingine amewapongeza wasomi hao kwa kuhitimu elimu ya vyuo vikuu akieleza kuwa ni jitihada kubwa wameifanya kufika hapo walipofikia huku akiwaomba wasikatishwe tamaa na yeyote wanaporejea mtaani.

“Mmeshapata elimu zenu sasa mnarudi mtaani, kule mtakuta watu wengi san, na siyo kila aliyepo mtaani amesoma, wengi wana elimu za kawaida tu na inawezekana wakawa wamekuzidini maarifa lakini nataka niwaambie mafanikio ya maisha yako unayo wewe mwenyewe, nendeni mkashirikiane na wananchi wenzenu vyema” Amesihi Kawaida.

Mwisho Kawaida amewasihi vijana kuendelea kuwa wamoja na kutokata tamaa kwani hata historia yake ya uongozi tangu alipomaliza elimu ya vyuo na vyuo vikuu ni matokeo ya kutokukata tamaa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!