Mwanamitandao na mtaalamu wa mawasiliano, Kennedy Mmari ametoa wito kwa Tanzania kuanzisha chombo maalum cha kudumu cha kufuatilia na kudhibiti mwenendo wa Jeshi la Polisi (Police Oversight Body) na Ofisi ya Ombudsman, ili kushughulikia na kuchakata malalamiko ya wananchi dhidi ya jeshi hilo.
Katika andiko lake katika mtandao wa X, lililozungumzia changamoto zinazokabili Jeshi la Polisi, Mmari amesisitiza kuwa hali ya taasisi hiyo kujichunguza yenyewe ni upungufu mkubwa katika mfumo wa haki nchini.
Mmari anasema kuwa ni hatari kwa taifa kuwa na taasisi inayotuhumiwa, lakini ikawa inajichunguza yenyewe na kujipeleka mahakamani yenyewe.
“Hatuwezi kuwa na taasisi ambayo ikituhumiwa, inajichunguza yenyewe na kujipeleka mahakamani yenyewe. Hizo ni sarakasi za kilaghai. Sisi wote, na si wananchi pekee, hata watawala, tupo kwenye hatari ya kuwa wahanga wa taasisi isiyoweza kudhibitiwa”, alisema Mmari, akionesha wasiwasi wake juu ya uwezo wa polisi kujichunguza bila kuwa na chombo huru cha kudhibiti mwenendo wake.
Akiendelea kufafanua, Mmari anaeleza kuwa wananchi na watawala wote wapo kwenye hatari ya kuwa wahanga wa taasisi isiyoweza kudhibitiwa. Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi lina rasilimali nyingi zinazoweza kuthibitisha iwapo tuhuma zinazotolewa dhidi yake ni za kweli au za uongo.
“Polisi wana kila aina ya rasilimali za kuthibitisha kuwa wametuhumiwa kwa uongo; magari yao, bajeti yao, bunduki zao, taaluma yao, na mitambo yao,” amesema Mmari.
Katika kutoa mifano, Mmari amesema kuwa ikiwa polisi wanatuhumiwa kwa kuteka, wanapaswa kutumia rasilimali zao kuhakikisha waliotekwa wanapatikana na watekaji wanatiwa mbaroni. Pia, kama polisi wanatuhumiwa kwa kuua, wapo katika nafasi nzuri kutumia uwezo wao kuwabaini wauaji na kuwafikisha mahakamani.
Mmari amehitimisha kwa kusema kuwa polisi wanaposhindwa kutoa ushahidi mbadala dhidi ya tuhuma zinazoelekezwa kwao, basi tuhuma hizo zinabaki na nguvu kubwa kuliko utetezi wowote mwingine.