Latest Posts

KESI YA LISSU: ASKARI MPELEZI WA MBEYA ‘ALIVYOKWAMA’ KUSOMA PGO YA KIINGEREZA MAHAKAMANI

Na; Mwandishi wetu

Kesi ya uhaini Na. 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu inaendelea tena leo, Alhamisi Februari 19.2026, kama ilivyo kawaida mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru

Kesi hiyo ambayo inasikilizwa kwa mfululizo, leo imekuja Mahakamani hapo kwaajili ya mashahidi wa Jamhuri kuendelea kutoa ushahidi wake, ambapo shahidi wa kwanza kwa siku hii, ambaye kimsingi ni shahidi wa 12 wa Jamhuri kwa ujumla wake ni Askari Polisi H. 937 Detective Koplo Vicent

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka, shahidi huyo ambaye ni Askari Polisi ameieleza Mahakama kuwa yeye ana umri wa miaka 36, Dini yake ni Mkiristo, Mkazi wa Mbeya na anafanya kazi zake Police Central Mbeya

 

Anasema yeye, alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 2011, ambapo alipata mafunzo ya awali ya Upolisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP Moshi) na kuhitimisha mafunzo hayo Machi 03.2012

 

Anasema baada ya kuhitimu rasmi mafunzo, akapangiwa Mkoa wa Mbeya, huku majukumu yake ya kila siku ikiwa ni kupeleleza kesi zinazofunguliwa pale kituoni, kukamata watuhumiwa na kutoa ushahidi Mahakamani

 

  1. 937 Detective Koplo Vicent ameieleza Mahakama kuwa mnamo Aprili 05.2025 akiwa anaendelea na majukumu yake ya kawaida kwenye Kituo cha Polisi cha Mwanjelwa, aliitwa na Mkuu wa Kituo na kupewa kazi ya kumtafuta ‘P9’

 

Anasema kulikuwa na taarifa fiche zilizoletwa kituoni hapo, zilizodai kuwa ‘P9’ anahamasisha kwenye vijiwe mbalimbali kuchochea Uchaguzi Mkuu wa 2025 usifanyike, ndipo akapewa maelekezo ya kumkamata

 

Anasema baada ya kupewa maelekezo hayo na Mkuu wa Kituo, Mkuu huyo wa Kituo pia alimpatia namba ya simu ya ‘P9’ ambapo Mkuu huyo wa Kituo alipata namba hizo za simu kutoka kwa msiri wake

 

Anasema kabla ya kumpigia na kumkamata, awali alimfuatilia na kugundua kuwa mtuhumiwa ni fundi Umeme, na ndipo yeye akatumia mbinu ya ‘kiupelelezi’ kumpigia mtuhumiwa huku akijitambulisha kuwa yeye ana tatizo linalohitaji fundi kama yeye kulitatua na wakakubaliana sehemu ya kukutana, na alivyofika alimueleza kuwa yeye si mteja kama alivyojitambulisha hapo awali, badala yake alijitambulisha kuwa yeye ni Askari Polisi (mpelelezi), akamuonesha kitambulisho chake cha kazi na kumueleza kuwa yuko chini ya ulinzi na kwamba anatuhumiwa kufanya uchochezi na kuhamasisha vurugu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025

 

Shahidi huyo ameendelea kuieleza Mahakama kuwa, baada ya kumkamata mtuhumiwa (P9) hakutumia nguvu kwani alikuwa muelewa,  akaongozananae na kumkabidhi kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa, na alipofika kituoni alimkabidhisha mtuhumiwa huyo kwa Mkuu wa Kituo aliyemtuma kazi awali, na yeye aliendelea na majukumu mengine, na huo ndio ukawa mwisho wa ushahidi wake Mahakamani,

 

Baada ya shahidi huyo wa 12 wa Jamhuri ambaye ni Askari Polisi H. 937 Detective Koplo Vicent kumaliza kutoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka, baadae Mahakama ilimpatia nafasi mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kumuhoji shahidi maswali ya dodoso (Cross Examination)

 

Lissu: Nasikia we ni Home Boy wangu?

 

Shahidi: Ndio, ni sahihi kabisa, mimi ni Home Boy wako

 

Baada ya hapo Lissu alimuuliza shahidi kama atayafahamu maelezo aliyoandika kama akionyeshwa, ndipo shahidi alikubali na Lissu akawaomba Majaji shahidi aonyeshwe maelezo hayo,

 

Aliponeshwa maelezo shahdii alikubali kuwa ni maelezo yake na hivyo Lissu aliiomba Mahakama kupokea kielelezo na yalipokelewa na kipewa jina D11

 

Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye maelezo yako kuna sehemu umeandika unafanya kazi Central

 

Shahidi: Hayapo

 

Lissu: Umesema tarehe 05/04/2025 ukiwa Kituo cha Polisi Mwanjelwa uliitwa na Mkuu wa Kituo ukiambiwa umtafute ‘P9’ kwa kosa la kuhamasha na kuchochea kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 usifanyike kwenye vijiwe mbalimbali, kweli si kweli?

 

Shahidi: Kweli

 

Lissu: Angalia kwenye maelezo yako

 

Shahidi: (anaangalia)

 

Lissu: Waeleze Majaji, nani aliyerekodi hayo maelezo yako?

 

Shahidi: Niliandika mimi mwenyewe

 

Lissu: Mtu anayeandika maelezo huwa anapewa onyo sio..

 

Shahidi: huwa hakuna onyo

 

Lissu: Hakuna maneno kama ‘nitasema kweli, kweli tupu nisiposema kweli nishtakiwe

 

Shahidi: Sio onyo

 

Lissu: huwa unasema nitasema kweli mbele ya nani?

 

Shahidi: mbele yangu mi mwenyewe..

 

Lissu: Nataka nijue huwa unasema mbele ya nani?

 

Shahidi: Kwa kuwa haya maelezo ni ya kwangu..sijakuelewa

 

Lissu: Hayo maneno unayatamka mbele ya nani?

 

Shahidi: Sio lazima utamke mbele ya mtu

 

Lissu: Unafahamu kitu kinaitwa PGO (Police General Order)?

 

Shahidi: Ndio naifahamu

 

Lissu: Kwenye PGO, ni kweli au si kweli kwamba PGO 236 inasema yeyote anayeandika maelezo ya ushahidi lazima aandikwe na askari anayefanya kazi hiyo?

 

Lissu akampa shahidi kitabu ch PGO,

 

Shahidi: Hii PGO mshtakiwa ni ya Kingereza sasa kwenye lugha ya Kingereza nisije nikakudanganya

 

Lissu: IGP alijua unafahamu Kingereza

 

Shahidi: Ya Kiswahili ipo

 

Lissu: Kwa hiyo huwezi ukajibu kwa sababu hujui Kingereza

 

Shahidi: Siwezi,

 

Lissu: Kwa mujibu wa PGO mtu ambae maelezo yanarekodiwa ya ushahidi hawezi akajiandikia maelezo mwenyewe

 

Shahidi: Sifahamu

 

Lissu: Kwenye ushahidi mwishoni umethibitisha ‘mimi kolo Vicent nathibitisha kuandika maelezo yangu kwa usahihi na uaminifu chini ya kifungu cha 10(3)(C) cha CPA RE.2022

 

Shahidi: Sahihi

 

Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye hiyo sheria kuna hicho kifungu

 

Shahidi: Haya maelezo nilipokuwa nayaandika 2025 hiki kifungu kilikuwepo

 

Lissu: Kilikuwepo?

 

Shahidi: Ndio

 

Lissu: Waeleze Majaji kama kuna mtu yeyote aliyeshuhudia ukiandika hayo maelezo

 

Shahidi:…

 

Lissu: Wakari unamkamata alikuwa anafanya kosa gani?

 

Shahidi: Alikuwa na kosa la kuchochea na kuzuia uchaguzi mkuu

 

Lissu: Ulimkamata akiwa anachochea?

 

Shahidi: Njama, kwa muda huo alikuwa hachochei

 

Lissu: Swali langu wakati unamkamata alikua anafanya kosa lolote

 

Shahidi: Alikuwa hafanyi kosa lolote

 

Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye maelezo yako umetaja jina la huyo Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa

 

Shahidi: Kwenye maelezo hakuna

 

Lissu: Na kwenye ushahidi wako umetaja jina?

 

Shahidi: Sijamtaja

 

Lissu: Umeeleza huyu mtuhumiwa P9 alikua anafanya/amefanyia kosa

 

Shahidi: Sikufafanua

 

Lissu: umesema alikua kwenye vijiwe

 

Shahidi:…

 

Lissu: Waheshimiwa Majaji namsomea shahidi maana ya kijiwe kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili iliyotolewa na BAKITA (Mahali ambapo watu hasa vijana wasio na kazi hukaa pasi kufanya kazi), swali langu Mbeya ina vijiwe vingapi?

 

Shahidi: Sifahamu

 

Lissu: Waeleze Majaji kama umetaja alikua ameenda kwenye kijiwe gani?

 

Shahidi: Sijataja

 

Lissu: Waeleze Majaji kama umetaja tarehe ya huyu P9 aliyofanya hayo makosa

 

Shahidi: Nimetaja tarehe 05

 

Lissu: Tarehe 05 ndio siku uliyotumwa ukammakate, tusipotezeane muda

 

Shahidi: Tarehe 05 siku hiyo hiyo

 

Lissu: P9 alipanga njama na nani?, maana njama haipangwi na mtu mmoja

 

Shahidi: haijaelezwa

 

Lissu: Kuna kosa katika nchi hii la kuzuia Uchaguzi?

 

Shahidi: kosa lipo

 

Lissu: Sheria gani?

 

Shahidi: Sheria ndo siijuwi lakini kosa lipo

 

Lissu: Nikikuambia kuwa kwa sheria za Tanzania, kuzuia Uchaguzi si kosa popote pale utabisha?

 

Shahidi: Kosa lipo

 

Lissu: Waheshimiwa Majaji naomba nimuoneshe shahidi Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 iliyosainiwa na ‘Mama’, na kwenye sheria hii hakuna sehemu yoyote iliyosema kuzuia Uchaguzi ni kosa

 

Shahidi: hilo sijuwi

 

Lissu: (anampatia shahidi Sheria ya kanuni ya adhabu aipitie na kueleza kosa la kuzuia Uchaguzi)

 

Shahidi: shahidi hii ni ya Kiingereza, kama kuna ya Kiswahili lete

 

Lissu: Ieleze Mahakaman kuwa P9 hakupelekwa Mahakamani kabisa?

 

Shahidi: Sijuwi, mimi jukumu langu lilikuwa kumfikisha kituoni

 

Lissu: unajuwa kwamba huyu P9 hakupelekwa Mahakamani popote badala yake amekuwa shahidi wa kesi hii?

 

Shahidi: sijuwi

 

Lissu: unajuwa kosa ambalo nimeshtanalo?

 

Shahidi: najuwa unashtakiwa kwa uhaini

 

Lissu: nimefanya matendo gani?

 

Shahidi: siyajuwi yote

 

Lissu: Umekuja kufanya nini?

 

Shahidi: kuna machache nafahamu

 

Lissu: Yapi

 

Shahidi: Nachofahamu ni kwanba unashtakiwa kwa kosa hilo kutojana na kauli zako

 

Lissu: Mimi natoa kauli kwa maelfu, unazungumzia kauli yani?

 

Shahidi: Video mojawapo ukihamasisha utakinukisha uchaguzi wa mwaka hu sijui utakuaje vitu kam hivyo

 

Lissu: Umeleta hiyo video Mahakamani?

 

Shahidi: Niliiona tu, sijaiwasilisha

 

Lissu: Waheshimiwa Majaji, sina maswali mengine

 

Baada ya mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kumaliza kuhoji maswali ya dodoso, Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka alimgeukia shahidi na kumuuliza ‘umeulizwa kuhusu takwa la onyo hebu ieleze Mahakama takwa la onyo huwa linatumika katika maelezo gani?

 

Shahidi katika majibu yake aliieleza Mahakama kuwa huwa linatumika katika maelezo ya mtuhumiwa, na yeye ameandika maelezo ya shahidi.

 

Kesi hiyo inaendelea ambapo shahidi wa pili kwa siku ya leo, ambapo kwa ujumla wake ni shahidi wa 13 wa Jamhuri anaendelea kutoa ushahidi, huyu ni shahidi wa siri, dereva Bodaboda kutoka Mbeya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!