Latest Posts

KESI YA UCHOCHEZI YA LISSU YASUKUMWA JULAI 1, JAMHURI YASUBIRI SHAHIDI WA MITANDAO

Shauri Na. 8606/2025 la uchochezi na kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa YouTube linalomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Antiphas Lissu limeahirishwa mpaka Julai 1, 2025 baada ya upande wa jamhuri kuomba ahirisho hilo.

Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga aliieleza mahakama kuwa shahidi Na.01 (aliyejitambulisha kama Inspekta John) aahirishe kutoa ushahidi mpaka pale Mtaalam Mchunguzi kutoka kitengo cha uchunguzi wa vifaa vya elektroniki atakapotoa ushahidi wake.

Awali shahidi huyo alipokuwa akitoa ushahidi aliieleza mahakama kuwa kupitia video iliyochapishwa na chombo cha habari cha Jambo TV ilichapisha maudhui kwa mfumo wa live (mbashara) ambayo ndani yake yalikuwa na maneno yenye kuonesha kuzua taharuki.

Shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa baada ya kusikia maneno hayo alitoa taarifa kwa kiongozi wake na ambapo aliamriwa kwenda kwa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum aitwaye SACP George na kumuelezea na kisha baadaye kupakua picha mjongeo(video) hiyo na kuikabidhi kanda maalum.

Shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa baadhi ya taarifa zenye viashiria vya uchochezi na kuzua taharuki ambazo zilizungumzwa na Lissu siku hiyo zilichapishwa katika kurasa za mitandao ya kijamii na vyombo vingine ikiwemo Clouds TV, Arusha One TV na The Chanzo.

Akiendelea kutoa ushahidi huku akiongozwa na Wakili Katuga, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama kusitisha utoaji wa ushahidi kwa shahidi wa kwanza mpaka pale shahidi wa pili, mtaalam mchunguzi kutoka kitengo cha uchunguzi wa vifaa vya elektroniki atakapokuja na kutoa ushahidi kupitia kielelezo ambacho kina picha zikimuonesha Lissu akitenda makosa aliyoshtakiwa nayo.

Pamoja na upande wa utetezi kupinga hoja hiyo wakiongozwa na Wakili Kibatala ukidai kuwa ni janjajanja za shahidi kupoteza muda. Akihojiwa nje ya mahakama hiyo Kibatala amesema wanamsubiri kwa hamu shahidi huyo na mashahidi wengine katika kesi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!