Latest Posts

KESI YA UHAINI YA LISSU YAKWAMA TENA, UPELELEZI WADAIWA KUTOKAMILIKA

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, imeendelea tena leo kwa kutajwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao, ambapo upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Yahya, aliomba Mahakama kuahirisha shauri hilo hadi tarehe nyingine kwa kuwa uchunguzi wa kesi hiyo haujakamilika. Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa vikali na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mpale Mpoki, waliodai kuwa kucheleweshwa huko si tu kunakwaza haki za mshtakiwa, bali pia hakuna mashiko kisheria ikizingatiwa kuwa ushahidi wa kesi hiyo umetajwa kuwa upo wazi kwenye mtandao wa YouTube.

Upande wa Jamhuri ulijibu kuwa sheria haiwalazimishi kueleza undani wa upelelezi, na badala yake walieleza kuwa pindi uchunguzi utakapokamilika, taarifa zitawekwa kwenye mfumo rasmi wa Mahakama na kupelekwa pia kwa mawakili wa utetezi.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini aliisihi Jamhuri kushughulikia kwa haraka upelelezi wa kesi hiyo, na kusisitiza kuwa ifikapo tarehe mpya ya kutajwa, Mahakama inatarajia kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 19, 2025.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mshtakiwa Tundu Lissu aligoma kushiriki kwenye shauri hilo kwa njia ya mtandao, ambapo Kamishna Msaidizi wa Magereza Juma Mwaibako aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa amegoma kufuatilia kesi hiyo kwa mfumo huo.

Katika kesi hiyo, Mawakili 18 wa utetezi wakiongozwa na Mpale Mpoki walihudhuria, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Mawakili 4 wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Yahya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!