Latest Posts

KIGOGO TARURA ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA MKEWE

Na Fredrizzo Samson – Mara.

Mwanamke aitwaye Rhoda Jonathan (46), mkazi wa Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoa wa Mara, ameuawa kikatili kwa kukatwa mapanga karibu mwilini kote usiku wa Alhamisi, Oktoba 23, 2025, nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara, marehemu alikuwa mke wa Mhandisi Wilson Charles, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Kagera. Wawili hao walibarikiwa watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba ambaye ni mlemavu wa viungo.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtu asiyejulikana aliruka ukuta na kuingia ndani ya nyumba ya marehemu kabla ya kutekeleza mauaji hayo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga, James Makuru Marwa, aliiambia Jambo TV kuwa alipokea simu kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Serengeti akimtaarifu kuhusu mauaji yaliyotokea nyumbani kwa familia ya Mhandisi Wilson.

“Nilipofika sikukuta mtu yeyote ilibidi nimpigie simu tena Mkuu wa Shule, mkuu alifika akiwa na mwanafunzi aliyekuwa amepanga kwenye nyumba ya Rhoda, aliyekwenda kumpatia taarifa. Tulipoingia chumbani tukaona mkono ukiwa chini, ilibidi nichukue tochi na kumulika kila sehemu ndipo nikauona huo mwili pembeni ya kitanda”, amesema Makuru.

Baada ya kubaini tukio hilo, Mwenyekiti huyo aliarifu Polisi ambao walifika eneo la tukio, kukagua nyumba na kuuchukua mwili wa marehemu kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.

“Nilipiga simu Polisi wakasema mtu asiguse hilo panga wakaja wakalichukua. Kwakweli kitendo hiki ni cha kinyama hakijawahi kutokea kwenye kata yetu, ndiyo tukio la kwanza ambalo limetokea ” amesema Mwenyekiti.

Kijana mwenye umri wa miaka 14, Mophati Mwita, ambaye alikuwa anaishi nyumbani kwa marehemu, amesema tukio lilitokea saa moja usiku wakati akiwa jikoni.

“Ilikuwa siku ya Alhamisi nilikuwa jikoni napika mida ya saa moja usiku, nilimuomba Musa Marwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Serengeti aliyepanga hapa nyumbani akawashe taa ya nje. Alipofika pale uani alimuona mtu ameingia ndani- mwanaume, akajiuliza mbona geti limefungwa! Amepitia wapi? Kumbe aliruka ukutani. Yule mtu akamwambia mbona nagonga geti hufungui? Yule mtu akauliza mama yupo? wakati anauliza, shangazi alikuwa ndani anaongea na simu, wakati yule mtu anaongea na mwanafunzi ghafla akafika mwanaume mwingine, aliposikia sauti ya shangazi akiongea na simu akaingia moja kwa moja hadi chumbani alikokuwa shangazi”

“Yule mwanafunzi akatoka mbio kwenda hadi shuleni kumtaarifu Mwalimu Mkuu kuwa kuna mtu kavamia nyumbani, shangazi alipiga kelele, sikuwa na la kufanya kwasababu mimi ni mdogo na nyumbani tulikuwa mimi, shangazi na mwanaye ambaye ni mlemavu pamoja na huyo mwanafunzi”, amesema Mophati.

Amesema baada ya kelele hizo, mwanafunzi huyo alikimbilia shuleni kumtaarifu Mwalimu Mkuu, na baadaye Polisi walifika eneo la tukio. Mophati ameeleza kuwa waliona sura za watu waliotekeleza tukio hilo, lakini hawakuwatambua.

Akizungumza na Jambo TV, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mume wa marehemu, Mhandisi Wilson Charles, anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

“Ndiyo, tunamshikilia juu ya tukio hilo na mpaka sasa jeshi linaendelea na kazi yake na tunaiomba jamii kupitia ninyi waandishi wa habari ijiepushe na vitendo viovu”, amesema Kamanda huyo.

Kwa sasa, Jambo TV imeweka kambi kufuatilia kwa undani mgogoro unaoendelea kati ya familia za pande mbili- upande wa marehemu na upande wa mume wake baada ya tukio hili kusababisha hali ya majonzi na taharuki katika jamii ya Serengeti.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!