Akiwa na umri wa miaka 37 tu, Mtanzania Edha Nahdi, mmiliki wa Kampuni ya Amson Group amefanikiwa kuinunua Kampuni ya Saruji ya Bamburi Cement kwa takriban dola milioni 180, sawa na shilingi bilioni 475 za Kitanzania.
Ununuzi huu unaweka rekodi mpya kama uwekezaji mkubwa zaidi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi, kulingana na taarifa mbalimbali za kiuwekezaji. Uwekezaji huu unazidi ule wa mfanyabiashara Rostam Aziz, ambaye amewekeza nchini Kenya kupitia kampuni yake ya Taifa Gas kwa dola milioni 130 za Kimarekani.
Mkataba wa ununuzi wa Bamburi Cement unachukuliwa kama uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi kutoka kwa kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Ununuzi huu utawezesha Amson Group kuendelea kupanua biashara zake zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amson Group, inayoongozwa na familia ya Nahdi, inafanya biashara katika nchi kadhaa ikiwamo Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Burundi. Sasa, kampuni hiyo inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki.

Katika taarifa yao, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kupitia Mkurugenzi Mkuu Bw. Raphael Maganga, wamemsifu Edha Nahdi kama kijana mwenye upeo mkubwa wa kibiashara, mwenye maono na uthubutu wa hali ya juu. TPSF imeeleza kuwa Nahdi ameiheshimisha Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa uwekezaji huu mkubwa.