Latest Posts

KILICHOJIFICHA ‘AGIZO LA KUBOMOLEWA GHOROFA KARIAKOO’ MIGOGORO MKUBWA WA KIFAMILIA

Ijumaa ya tarehe 20 Disemba 2024, Mtaa wa Aggrey na Msimbazi Kariakoo kulifanyika zoezi ya kile kilichoitwa ‘ubomoaji wa jengo la ghorofa kwa kuwa limechakaa’ ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo vifo iwapo ghorofa hilo litaporomoka.

Aliyetoa agizo hilo ni Warda Abdallah Bahashwan ambaye ni mmoja wa wamiliki wa jengo hilo ambalo linamilikiwa na watoto watano wa kike wa marehemu Abdallah Mohammed Bahashwan, Wamiliki wengine ni Faiza, Jamila Sabaha na Fatma Abdallah Bahashwan.

Sasa tutafakari Warda anasema msimamizi wa Jengo hilo anazuiwa kuvunja. Huyu anayesemwa msimamizi ni Arafat Abdallah Bahashwan ambaye ni mtoto wa mwisho wa Bahashwan lakini si mmiliki na hatambuliki katika mirathi kulingana na nakala za kisheria ambazo Jambo TV ilizinasa.

Warda Abdallah Bahashwan

Je kwa nini Warda alikuja yeye kama mmiliki mmoja? Kwanini wapangaji hawakupewa notisi ya angalau siku 14? Kwanini aliita vyombo vya habari kuja kushuhudia akitaka kuvunja? Kwanini alikuja na kampuni binafsi ya ulinzi wakiwa na silaha kama bunduki pamoja na mbwa? Kwa nini wavunjaji hawakuvaa kifaa chochote cha kuwalinda ikiwemo helmeti? Kwa nini siku mbili baada ya Arafat kukamatwa kwa kusababisha vurugu, itoke taarifa kupitia chombo kimoja cha habari kuwa “DC Mpogolo kwa nini unaagiza mtu ashikiliwe saa 48?”

Maswali haya yawe kiini cha makala hii kwani kuna mengi ya kufahamu.

Ni kweli Warda ni sehemu ya wamiliki wa jengo hilo kati ya wamiliki watano lakini suala la kutaka kubomoa bila ushahidi wa makubaliano na wenzie linaleta ukakasi.

Warda alimtaja Arafat kama msimamizi lakini ikumbukwe Jambo TV ndiyo iliibua mgogoro wa jengo hili kwa mara ya kwanza na ifahamike ni mgogoro wa zaidi ya miaka 10 tangu mwaka 2013. Kulingana na taarifa, Arafat ni mtoto wa mwisho kwa familia ya Abdallah Bahashwan na yeye sio sehemu ya wamiliki wa jengo hilo, hata hivyo alikuwa anasimamia milango (fremu) za dada yake ambaye niWarda kwa sababu Warda anaishi nje ya nchi.

Sasa baadaye ikaelezwa kuwa aliingiwa na tamaa ya kutaka kumlaghai dada yake ambaye hawezi kuongea na hasikii(lakini ni mzima wa akili) aitwaye Jamila kwa kutaka kodi za huyu Jamila achukue yeye. Hayo yalileta shida na ndugu wengine.

Utaratibu wa kuvunja majengo hasa yaliyopo mjini lazima uwe na kibali kutoka ardhi lakini pia wapangaji wapewe notisi ya siku angalau 14. Haijulikani kwa namna gani ila Arafat aliwahi kuwa na kibali cha kuvunja jengo hilo na aliwaandikia wapangaji notisi waondoke. Kibali hicho kilizuiliwa na jiji kupitia barua iliyotoka tarehe 04/07/2024 na Arafat aliipokea na kusaini tarehe 18/07/2024.

Hapa napo kuna maswali, Warda anaeleza kuwa wana kibali tangu mwezi wa sita, je hafamu kuwa kilizuiliwa? Lakini tarehe 14/07/2024 Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa Dar Es Salaam Shukran Kyando alifika pale kwa maagizi ya Waziri wa Ardhi wa wakati huo Jerry Silaa na kutoa tamko kuwa hakuna nyaraka ambayo inamtambua Arafat kama mmiliki aache mara moja usumbufu na hatua zingine ikiwemo Arafat kwenda kuhojiwa zilifanyika.

Kuhusu kutaka kuvunja jengo na akaenda na kampuni binafsi ya ulinzi wakiwa na silaha kama bunduki pamoja na mbwa hili nalo linatia ukakasi mkubwa. Wapangaji wa jengo lile wanadai kuwa na hofu sana kutokana na namna wavunjaji walivyokwenda. Lakini je unapotaka kumchinja kuku wako kuna haja ya kumlenga ili umvunje miguu? hapana inahitaji kumtupia mahindi umuite bandani kazi imeisha. Mmiliki wa jengo alienda na silaha ili kuwatisha wapangaji au wamiliki wenza?

Jambo TV imemtafuta Sabaha Bahashwan ambaye ni sehemu ya wamiliki akahoji juu ya uvunjaji akasema “tunashangaa Warda anatamka yeye kapewa idhini na kabarikiwa ule ubomoaji ufanyike siku ile, sasa vibali hivi alivyopewa mbona sisi wamiliki wanne hatujaviona”

Sabaha Abdallah Bahashwan

“Sisi ni wamiliki hapo tittle deed (nyaraka zinazoonesha umiliki) zipo tano hazipo nne, wa sita anayetaka kumpenyeza hayumo mbona sisi wanne hatujatafutwa na tupo hai na tupo Dar es Salaam, mmoja wetu tu Fatma ndiye anaishi nje na taarifa zetu serikali wanazo; mawasiliano, na tunapoishi”. Anasema Sabaha.

Kwa uchunguzi wa Jambo TV inadaiwa kuwa kuna mwekezaji (Don) anataka kujenga jengo kubwa la ghorofa zaidi ya 10 kwenye kiwanja hicho kwa kuwa ni ‘potential’ hivyo anamlaghai ndugu mmoja na dada ili kupata eneo hilo.

Kuna shutuma dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo kuzia jengo hilo lisibomolewe. Jambo TV imezungumza na Sabaha ambaye ndiye amekuwa akifika kwenye jengo mara kadhaa kuzuia uvunjaji tukamuuliza kuhusu la DC Mpogolo akakiri ni kweli amewasiliana na DC siku ya tukio.

Sabaha akaeleza kuwa DC Mpogolo hahusiki kwa vyovyote na kuzuia uvunjaji bali alituma mgambo na askari kuzuia hali ya vurugu na uvunjifu wa amani uliokuwa unafanyika pale Kariakoo. Kwa sababu pia DC anaufahamu mgogoro huo vyema.

Ni vyema serikali ikachukua hatua ya kufahamu na kufuatilia mgogoro huu ambao upo katika eneo muhimu kibiashara lakini pia unahusisha mtu aliyepo katika kundi maalum la ulemavu.

Mahojiano ya Sabaha yapo Youtube ya Jambo TV.

Baadhi ya video kuhusu jengo hili zipo youtube ya Jambo TV kupitia link hii hapa

https://youtu.be/bD_wsFPpahc?si=keqS3rzVEOHQvCo8

https://youtu.be/6aSMjvvBTHQ?si=Ea8OpX66Y0DBCvs-

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!