Wakazi wa Kipunguni, kata ya Kipawa, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam wamesema wamechoshwa na ahadi za muda mrefu kutoka serikalini ambapo wakazi hao wanadai fidia zao kufuatia kuachia eneo hilo (Kipunguni) kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
Jambo TV imeshuhudia kilio cha wakazi hao wakiwemo wanawake na wazee waliokuwa wanawasilisha kero hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo aliyeitisha mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi, mkutano uliofanyika uwanja wa Banana Wakicha, kata ya Kipawa.
Katika maelezo yao wakazi hao wamedai kuwa wamezuiliwa kufanya shughuli zozote za maendeleo kwenye eneo hilo tangu mwaka 1997, hata hivyo kufuatia ukimya wa muda mrefu baadaye serikali ilianzisha mchakato wa kulipa fidia kupitia tathmini ya awali jambo ambalo iliilazimu Mahakama kuingilia Kati na kuiamuru serikali kufanya tathmini upya ili fidia hiyo ilipwe kulingana na thamani ya wakati husika
Baada ya amri hiyo ya Mahakama, inaelezwa kuwa serikali ilifanya tathmini upya Julai 2021 ambapo wananchi hao waliahidiwa kulipwa fedha zao haraka iwezekanavyo jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa
Katika kufuatilia jambo hilo wakazi hao kutoka kwenye kaya 1864 wamefika kwa viongozi mbalimbali wa serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa ngazi mbalimbali ikiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa Amos Makalla nk, lakini kote huko walipewa ahadi na maneno ya matumani ambayo hayajatekelezwa hadi sasa
Aidha, wakazi hao walioko kwenye jimbo la Segerea wameendelea kudai kuwa kwa sasa wanataka kusikia kauli ya moja kwa moja kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa hawana imani na viongozi wengine
Wamesema Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ni miongoni mwa viongozi waliotoa ahadi nyingi kwa wananchi hao bila utekelezaji, kwa kuwa mara nyingi amezungumzanao kwa kufanya mikutano ya hadhara au kupigiwa simu na kutolea ufafanuzi kwa nyakati tofauti, ambapo mara ya mwisho alipigiwa simu na Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM Taifa Amos Makalla aliyekuwa kwenye mkutano wa hadhara kwenye eneo hilo
Inaelezwa kuwa katika majibu yake Waziri Mwigulu Nchemba aliahidi kuwa fidia hiyo ingelipwa kuanzia mwanzoni mwa mwezi wa nane katika mwaka huu mpya wa fedha 2024/25 lakini imekuwa kimya hadi sasa, hali iliyopelekea wananchi kufika kwenye mkutano huo wa Mkuu wa wilaya wakiwa wamebeba mabango ya malalamiko
Wananchi hao wamesema kwa muda mrefu tangu walipozuiliwa kufanya shughuli za maendeleo kwenye eneo hilo wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, elimu nk kutokana na kutokuwepo kwenye eneo hilo
Akizungumza na wananchi hao Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo pamoja na mambo mengine amewaeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Amesikia kilio chao hivyo ameagiza kuwa wananchi hao walipwe fidia/hela zao haraka iwezekanavyo, na kwamba katika maelezo yake amefafanua kuwa sasa rasmi wananchi hao watalipwa fedha hizo mwezi Oktoba mwaka huu (2024)
Kama haitoshi Mpogolo amezitaka Kamati mbili (2) za wananchi hao walizozichagua kufuatilia jambo hilo tangu mwanzo zifike kwenye ofisi yake (Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ilala) Jumanne ya wiki ijayo ili wakapokee taarifa na utaratibu utakaotumika katika malipo na kisha wakirejea wawaeleze wananchi wengine
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya huyo amewapongeza wananchi hao kwa uvumilivu wao wa muda mrefu wa jambo hilo, sambamba na kuwaleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana mapenzi mema na wananchi hao na ndio maana yuko tayari wakati wote kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.