Na Josea Sinkala, Mbeya.
Kutokana na kutembea umbali mrefu wa kilomita kumi kwa watoto wa vitongoji vya Ihombe, Iwala na Idugumbi kufuata elimu ya sekondari mjini Mbalizi, Serikali imejenga Shule ya Sekondari Ihombe ambayo inatarajiwa kufunguliwa Januari 2025.
Serikali inajenga shule ya sekondari Ihombe kwa gharama ya zaidi ya shilingi million 500.5 zilizotolewa katika Halmashauri ya Mbeya katika kitongoji cha Ihombe kata ya Utengule Usongwe ambapo pia wananchi walitoa nguvu zao pamoja na kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mpya.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ihombe, Mwalimu Zakia Hassan Mwangu, akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo ameishukuru serikali kwa kutoa fedha shilingi milioni mia nane themanini na tatu kwa ajili ya kujenga shule hiyo ambayo ilianzishwa kwa nguvu za wananchi.
Mwalimu Zakia anasema ujenzi huo uliokaguliwa na mkuu wa mkoa wa Mbeya umefikia hatua mbalimbali kwa majengo ya madarasa, ofisi na vyoo, jengo la utawala ambapo hadi kufika Januari 2024 ujenzi utakuwa umekamilika ili wanafunzi kuanza masomo kitongojini hapo.
Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza, amesema ni muhimu kuwekeza katika elimu hivyo kuipongeza Serikali Kuu kwa uamuzi huo wa kuboresha miundombinu ya elimu na kujenga shule mpya huku akihimiza ujenzi wa mabweni ambapo ameahidi kutoa shilingi million tano kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mabweni shuleni hapo.
Akizungumza na mamia ya wananchi, mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera, amesema ni dhamira ya Serikali kuboresha sekta ya elimu nchini kwa maendeleo ya Taifa.
Homera ameelekeza shule hiyo mpya ya sekondari Ihombe kuhakikisha inaanza Januari 2025 kama ilivyokusudiwa kwa kuanza na wanafunzi wasiopungua miambili.