Latest Posts

KIONGOZI WA CHADEMA AMZUIA KIONGOZI MWENZIE KUFANYA MKUTANO WA HADHARA KATAVI

Katika tukio lililoonekana kushtua mioyo ya wafuatiliaji wa siasa za vyama ndani ya mkoa wa Katavi na Tanzania kwa ujumla, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Magharibi, Masanja Mussa Katambi, alizuia mkutano wa hadhara wa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Katavi, Rhoda Edward Kunchela.
 
Tukio hilo lilitokea Jumatatu, Oktoba 7, 2024, katika Kata ya Kakese, Manispaa ya Mpanda Mjini, ambapo Kunchela alikusudia kusikiliza kero za wananchi.
 
Inadaiwa kuwa chanzo cha mvutano huo ni uhusiano wa kifamilia kati ya Katambi na Diwani wa Kata hiyo aliyetajwa kwa jina la Maganga Mussa Katambi, ambaye ni mdogo wake wa damu.
 
Maganga, ambaye pia ni Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda, ametajwa kushirikiana na kaka yake kufanya vitendo vya kihalifu katika kata hiyo, vitendo ambavyo vimeelezwa kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi.
 
Jambo TV tulimtafuta Rhoda Kunchela kueleza kipi hasa kilijiri ambapo kwa maelezo yake amedai kushangazwa na tukio la kuzuiwa kufanya mkutano licha ya polisi kuridhia ombi la kufanya mkutano huo.
 
Amesema walipowasili Kata ya Kakese, walikumbana na vizuizi vya magenge ya ‘kihuni’ ambayo yalizuia gari la kwanza la muziki, walipokodi gari jingine, wamiliki walihongwa ili wasitishe huduma, na hivyo kulazimika kutumia gari la tatu.
 
“Tulipofika kwenye hiyo kata tukakutana na mazuio ya magenge ya kihuni ambayo yalikuwa yamesimama barabarani, wakazuia gari ya kwanza ya muziki, tukakodi gari nyingine wakamhonga mwenye gari hela akawa amekataa, baadaye tukapata gari nyingine”, ameeleza Rhoda.
Kunchela amefichua kuwa kabla ya mkutano, Masanja aliwapigia simu baadhi ya viongozi wa kata na kuwaonya kuwa vurugu zitazuka, akiwatisha kuwa watapata madhara, na hayoo aliyafahamu katika kikao cha ndani na viongozi hao.
 
Kunchela amedai kumekuwa na maovu yanayofanywa ndani ya kata hiyo, ikiwemo mateso kwa wananchi, malipo ya faini kinyume na sheria, na mauaji ya kiholela. Hali hiyo imewaweka wananchi katika hofu, huku wakishindwa kuripoti uhalifu kwa polisi kutokana na vitisho vya viongozi wa kata.
 
Kunchela amesisitiza kuwa Masanja hana mamlaka ya kikatiba kumzuia kufanya mkutano wa chama, na kwamba yeye anawajibika kwa Mwenyekiti wa Kanda pekee. Ameeleza kuwa tayari taarifa imetolewa kwa chama, na hatua zaidi za kinidhamu zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya Masanja.
 
“Tumeamua kutoa taarifa kwenye chama ninadhani hatua nyingine itakuwa kichama zaidi kwa maana taarifa anayo katibu mkuu wa chama, watajua watamuwajibisha namna gani kutokana na kitendo chake cha kuzuia mkutano”, ameeleza Kunchela.
 
Jitihada za kumtafuta Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Magharibi zinaendelea ili naye apate wasaa wa kuzungumzia sakata hilo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!