Baada ya kuibuka kwa minong’ono na maswali lukuki kuhusiana na ukimya wa Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda hatimaye Katibu Tawala wa mkoa huo Missaile Mussa ametegua kitendawili hicho kwa kueleza kuwa kiongozi huyo kwa sasa yuko likizo
Akihojiwa kwa njia ya simu na mwandishi wa habari Global TV online Julai 26.2024 Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Missaile Mussa amesema hana taarifa za ziada tofauti na hizo ya kwamba Makonda yuko likizo na kwamba si jukumu la Katibu Tawala wa mkoa kujuwa nini kinaendelea au kinafanywa na mtu aliyeko likizo.
Siku za hivi karibuni kumÄ™kuwa na minong’ono na maswali lukuki yanayotengeneza sintofahamu na pengine wasiwasi miongoni mwa jamii kuhusiana na ukimya wa takribani majuma mawili (2) wa Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda, ambapo ukimya huo umetafsiriwa kuwa si wa kawaida kutokana na haiba ya kiongozi huyo hasa katika utendaji wake wa kazi ambapo mara zote pindi anapokuwa ofisini ni lazima atafanya jambo linalohusisha jamii moja kwa moja, hivyo ukimya wake kuibua maswali na wengi wakitaka kufahamu ni wapi aliko na ukimya wake unaashiria nini
Aidha, maswali na minong’ono hiyo iliongezeka zaidi baada ya hivi karibuni kushuhudiwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akikaimu kiti cha Mkuu wa mkoa wa Arusha, kwa kuwa mara ya mwisho Makonda kuonekana hadharani ni pale alipofunga mashindano ya mbio za Pikipiki za ‘Samia Motocross Championship 2024’ zilizofanyika viwanja vya Lakilaki, Kisongo, jijini Arusha
Pasi na shaka majibu ya Katibu Tawala mkoa wa Arusha Missaile Mussa yataondoa maswali na minong’ono iliyokuwemo miongoni mwa jamii kuhusu ukimya wa Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda