Latest Posts

KITEREJA: MAPINDUZI YA ELIMU YA KKK KUWAJENGEA WATOTO KUJIAMINI

Montessori Community Tanzania yaunga mkono mageuzi ya elimu ya awali, kupitia uzinduzi wa mpango mkakati wa kisayansi wa kumjengea mtoto umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali pamoja na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.

Mpango huo umezinduliwa, Januari 29, 2026, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Montessori Community Tanzania, Bi. Sara Kitareja, amesema mpango huo ni wa kihistoria na umefika katika wakati muafaka, akibainisha kuwa kwa muda mrefu wadau wa elimu wamekuwa wakisubiri mpango unaomuwezesha mwalimu kufundisha kwa vitendo na kwa ubunifu zaidi.

Amesema mpango huo utamwezesha mwalimu kutengeneza na kutumia vifaa vya kufundishia vinavyoendana na mazingira ya darasani, jambo litakaloongeza ufanisi wa ujifunzaji kwa watoto kuanzia ngazi ya awali.

Bi. Kitareja ameeleza kuwa mbali na kuwajengea watoto uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu, mpango huo pia unalenga kuwajengea stadi muhimu za karne ya 21, ikiwemo mawasiliano bora, kujiamini, ubunifu pamoja na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali.

“Huu ni mpango unaomuweka mtoto katikati ya ujifunzaji. Watoto watajifunza kwa vitendo, jambo linalochangia maendeleo yao ya kiafya, kiakili na kimwili,” amesema.

Ameongeza kuwa wadau wa elimu nchini wanaunga mkono mpango huo kwa asilimia 100, wakiamini kuwa changamoto ya watoto kufika darasa la tatu bila ujuzi wa kusoma na kuandika itaondoka iwapo walimu watapatiwa mafunzo sahihi pamoja na miongozo ya kitaalamu.

Kwa mujibu wa Bi. Kitareja, mpango huo pia utamjengea mwalimu uwezo wa kuongeza ubunifu katika ufundishaji na kumwandaa mtoto kwa misingi imara ya elimu, huku akisisitiza kuwa vifaa vitakavyotengenezwa vitakuwa jumuishi na vitatumika kwa watoto wa aina zote bila ubaguzi.

Aidha, amesema Montessori Community Tanzania tayari imeanza kuunga mkono utekelezaji wa mpango huo hata kabla ya uzinduzi wake rasmi, baada ya kuingia makubaliano ya ushirikiano (MOU) na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

“Kupitia ushirikiano huu, tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na walimu wa elimu ya awali wilayani Mkalama, tukiwajengea uwezo wa kutengeneza zana za kufundishia pamoja na kutumia mbinu bora za kumlea na kumfundisha mtoto,” ameongeza

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!